Sera, siasa za ulimwengu zinavyoathiri mapambano

Ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya mwaka 2023 ilionyesha mauzo ya nje ya makaa ya mawe yaliongezeka mara tatu zaidi hadi kufikia Dola za Marekani milioni 299 (Sh807.3 bilioni) mwaka wa fedha 2022/23 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ongezeko hilo lilitokana na mahitaji zaidi ya makaa hayo duniani, kufuatia upungufu wa usambazaji wake uliosababishwa na vita ya Ukraine.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa uzalishaji ulifikia tani milioni 2.51 mwaka 2022 ikilinganishwa na tani 976,319 mwaka 2021 na wastani wa tani laki tano miaka mitano iliyopita.

Mshauri wa Masuala ya Uwekezaji na Biashara za Kimataifa, Reselian Manaiya anasema nchi za Ulaya zilitegemea gesi kwenye uzalishaji wake wa nishati na Russia ilichangia asilimia 70 ya usambazaji wa nishati hiyo.

“Vita imesababisha nchi hizi ziweke vikwazo kwa Russia na hivyo kupunguza utegemezi,” alisema na kuongeza nchi hizo zilihitaji vyanzo vingine vya nishati, akitolea mfano kuwa ongezeko la uzalishaji wa makaa ya mawe nchini ukiashiria hilo.
Makaa ya mawe nchini yanazalishwa kwa kiwango kikubwa katika Mkoa wa Ruvuma, maeneo ya Ngaka na Mbalawala, na Mbeya kuna mgodi wa Kiwira. Kwa mujibu wa Wizara ya Madini, bidhaa hiyo husafirishwa nje ya nchi kwa nchi za Afrika, Ulaya na kwingine.

Licha ya ukweli kwamba sayansi inaonyesha wazi nishati kusukuku (makaa ya mawe, mafuta na gesi asilia) ni kichochezi kikubwa cha mabadiliko ya tabianchi, dunia bado inaongeza uzalishaji wake.

Mhadhiri katika Kituo cha Mafunzo ya Mabadiliko ya Tabianchi cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Pius Yanda anasema zaidi ya asilimia 70 ya hewa joto inatokana na matumizi ya nishati chafu na ukataji miti ukichangia kwa asilimia 25.

Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (UNEP) unakiri, “Nishati ya kisukuku ndiyo kichocheo kikuu cha mabadiliko ya tabianchi. Kupunguza uzalishaji na matumizi kwa angalau asilimia sita kwa mwaka ni muhimu ili kuepusha hali mbaya zaidi za ongezeko la joto duniani.”

Takwimu za Wakala wa Kimataifa wa Nishati (IEA), kwenye ripoti ya Mapitio ya Nishati ya Dunia (WEO) 2023, zilibainisha uzalishaji wa makaa ya mawe uliongezeka hadi tani bilioni 6.1 mwaka 2022 ikilinganishwa na wastani wa tani milioni mbili mwaka 2000.

Vilevile mafuta yalizalishwa hadi tani milioni 4.52, ongezeko la zaidi ya asilimia 40 na gesi ikifikia tani milioni 3.71. Kiwango hicho kinatajwa na ripoti hiyo kuwa cha juu zaidi cha uzalishaji kwenye historia ya dunia.

Haya yanatokea licha ya nchi kupitia Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) kwenye mkutano wa Paris COP21 mwaka 2015 ambapo nchi zilikubaliana kupunguza uzalishaji wa hewa joto kwa kupunguza matumizi ya nishati kisukuku zinazozalisha hewa hizo kwa kiasi kikubwa.

Malengo yalikuwa kudhibiti ongezeko la wastani wa joto duniani libaki chini ya nyuzi joto za sentigredi 1.5 mpaka 2030, kwani kwa mujibu wa UNFCCC, dunia ipo sentigrade 1.1 mwaka 2023.
Hata hivyo, tafiti zinakadiria nchi zitaendelea kuzalisha nishati hizo.

Mfano mtandao wa Covering Climate now ulinukuu Gazeti la New York Times lililoripoti “ikiwa makadirio ya sasa yatatokea mpaka Mwaka 2030, Marekani itachimba mafuta na gesi zaidi kuliko wakati wowote katika historia yake. Russia na Saudi Arabia zinapanga kufanya vivyo pia”.

Mtandao huo ulitaja uwepo wa miradi 422 ya mafuta, gesi na makaa ya mawe ambayo inafanya kazi na inazalisha hewa joto, kiwango kinachoondoa kabisa matumaini ya kuzuia ongezeko la joto chini ya nyuzi joto 1.5°C.

Nchi haziwajibiki licha ya makubaliano

Kwa mujibu wa tovuti ya UNFCCC, hakuna sheria za moja kwa moja zinazolazimisha nchi kuachana na matumizi ya nishati chafu wala kulazimisha nchi kulipa fidia kwa uchafuzi walioufanya.

Tovuti hiyo inanukuu, “Makubaliano ya Paris, yanayolenga kudhibiti ongezeko la joto duniani kuwa chini ya nyuzi 2°C, ni mkataba wa hiari. Kwa mkataba huu, nchi zinajiwekea malengo yao ya kitaifa ya kupunguza uzalishaji wa gesi chafu (NDCs) na wanatakiwa kutoa taarifa kuhusu maendeleo yao bila shuruti ya kisheria ya kukataza kabisa matumizi ya nishati chafu”.

Profesa Yanda alisema jambo litakalowafanya wawajibike ni diplomasia, ndiyo sababu ya uwepo wa mkutano mkubwa wa nchi wanachama na kuongeza kuwa hii ni miongoni mwa hoja muhimu ambazo nchi inapaswa kuchukua kama ajenda.

“Nchi za Afrika ndizo zinazoathirika zaidi, licha ya mchango wake kuwa mdogo kwenye uchafuzi. Sababu kubwa ni mapinduzi ya viwanda na nchi hizo zinakiri na ziliahidi kutoa Dola za Marekani 100 bilioni kila mwaka, japo hazikufanya hivyo,” alisema.

Ripoti za IEA na World Energy Council, 2023 zinataja sababu za kama uchumi wa nchi hizi unategemea sana nishati hizo, ambazo yanatoa nishati kwa sekta nyingi, kama vile viwanda, usafiri, na miundombinu. Pia kuhama kwenda nishati mbadala ni gharama kubwa na inahitaji muda mrefu, jambo linalosababisha nchi nyingi kuwa na wasiwasi kuhusu madhara ya kiuchumi.

Sababu nyingine ni, “uhakika wa nishati muhimu kwani nchi hizi zinategemea nishati hizi kwa kuwa ni urahisi na gharama nafuu wa upatikanaji wake wakati nishati mbadala ikikabiliwa na changamoto za kutegemea hali ya hewa na teknolojia.”

Historia na madhumuni ya mkataba wa nishati

Mkataba huu ulianzishwa mwanzoni mwa miaka ya 1990 kwa lengo la kuweka ushirikiano wa nishati kati ya nchi zenye nishati nyingi kama zile zilizokuwa sehemu ya Umoja wa Kisovieti (USSR) na nchi za Ulaya Magharibi.

Mshauri wa uwekezaji, Reselian Manaiya, anabainisha kuwa mkataba huu uliundwa katika mazingira ya kisiasa ya wakati huo, baada ya Vita Baridi, ambapo lengo lilikuwa ni kuhakikisha upatikanaji wa nishati kwa bara la Ulaya. Hata hivyo, hivi sasa mkataba huu umegeuka kuwa kizingiti katika juhudi za kimataifa za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Mkataba huu unalinda kampuni zinazozalisha mafuta na gesi asilia kutoka mashirika ya kimataifa kwa kuwawekea kinga dhidi ya sheria kali za mazingira zinazoweza kupitishwa na nchi wanachama,” anasema Reselian.

Wadau hawa wanashauri Tanzania kupuuza mkataba huu unaoungwa mkono na baadhi ya nchi za Ulaya na Asia.

Changamoto za kisera, sheria na siasa za ulimwengu

Mkurugenzi wa Muungano wa Asasi za Kiraia na Vyama vya Wafanyakazi vinavyofanya uchambuzi wa sera za uwekezaji na biashara nchini (Tanzania Trade and Investment Coalition – TATIC), Olivia Costa anasema licha ya maboresho yaliyofanyika kwenye ECT mwaka 2018, changamoto kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi hazikushughulikiwa ipasavyo.

Hii imefanya baadhi ya nchi kama vile za Umoja wa Ulaya kutangaza mpango wa kujitoa kwenye mkataba huo, zikiuona kama kikwazo kwa utekelezaji wa Mkataba wa Paris wa mwaka 2015.

Olivia anaongeza, “Kwa Tanzania, kujiunga na mkataba huu ni sawa na kujitia mtegoni. Rasilimali za mafuta na gesi asilia ambazo bado hazijachimbwa kikamilifu zinaweza kuzuiliwa kutumika kwa maendeleo ya kiuchumi kwa kuogopa migogoro ya kisheria na wawekezaji wa kimataifa”.

Mikataba hii na mikataba mingine inayolenga kuvutia uwekezaji kama ile ya Uwekezaji kati ya Nchi Mbili (MIUMBI) lakini tafiti zinaonyesha sio lazima iwe hivyo.

Uchambuzi uliofanywa na TATIC ulibainisha katika miaka 10 iliyopita Tanzania imepoteza zaidi ya Sh2 trilioni kutokana na kushindwa kesi za kiuwekezaji kwenye Mahakama ya kimataifa ya usuluhishi wa migogoro ya uwekezaji (ICSID). Kesi nyingi zilihusisha mikataba ya MIUMBI.

Mfano wa kesi za hivi karibuni ni ile ya Kampuni ya Symbion na Shirika la Umeme (Tanesco) ambapo serikali ililipa zaidi ya Sh352.9 bilioni, fedha nyingine zaidi ya Sh823 bilioni kwenye kesi tatu, ile ya Mikindani Estate ya Sunlodge na mbili dhidi ya Standard Chartered Hong Kong.

Vilevile tafiti zinaonyesha licha ya mikataba ya aina hii kusainiwa kwa dhana ya kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja (FDI), si mara zote huwa hivyo.

Mchambuzi wa mikataba kutoka TATIC, Ezekiel Kereri anasema sababu za masingi ni, “Usalama wa kisiasa, upatikanaji malighafi, upatikanaji wa wafanyakazi wajuzi na uongozi wa sehemu husika”.

Kereri anatoa mfano wa Benki ya Muhlberger for Deutsche iliyofanya tafiti kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara (SSA) zinachangia asilimia 12 ya watu duniani na asilimia 60 ardhi inayofaa kwa kilimo, asilimia 39 ya rasilimali za madini muhimu kama Cobald.

“Hata hivyo, licha ya kuwa na rasilimali hizi, SSA inachangia tu asilimia mbili ya biashara yote duniani, asilimia mbili ya Pato la Taifa la Dunia (GDP), asilimia moja ya uzalishaji wa viwandani na asilimia 3 tu ya mtiririko FDI duniani,” anasema.

Related Posts