Shamim, mumewe wakwaa kisiki Mahakama ya Rufani

Arusha. Mahakama ya Rufani imebariki adhabu ya kifungo cha maisha iliyotolewa kwa wanandoa, Shamim Mwasha na mumewe Abdul Nsembo waliohukumiwa baada ya kupatikana na hatia ya makosa ya kusafirisha dawa za kulevya.

Machi 31, 2021 wanandoa hao walihukumiwa adhabu hiyo na Jaji Elinaza Luvanda wa Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu uchumi.

Shamim anayemiliki blogu ya 8020 na mumewe Nsembo, ambaye ni mfanyabiashara, walikuwa wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kusafirisha gramu 280.4 za heroini Mei mosi, 2019, katika eneo la Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.

Baada ya kuhukumiwa adhabu hiyo, wanandoa hao hawakuridhika na kukata Rufaa katika Mahakama ya Rufani iliyoketi Dar es Salaam.

Jopo la majaji watatu wa Mahakama hiyo ambao ni Dk Mary Levira, Abdul-Hakim Amer Issa na Mustapha Ismail wametoa hukumu na kubariki adhabu hiyo Novemba 14, 2024 na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa mahakama.

Katika rufaa hiyo, warufani walikuwa wanadai mahakama ilikosea kisheria kutegemea ushahidi unaotokana na upekuzi usio halali, mahakama kukosea kisheria kushindwa kuzingatia utetezi wao, mahakama haikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na kesi dhidi yao haikuthibitishwa pasipo kuacha shaka.

Katika hukumu, Jaji Levira amesema kwa kuwa hoja ya sita ni kuwa mahakama iliyosikiliza kesi hiyo haikuwa na mamlaka, wana wajibu wa kuanza nayo kabla ya kushughulikia sababu nyingine.

 Hata hivyo, walihitimisha hoja hiyo kwa kueleza kuwa mahakama iliyosikiliza kesi hiyo ilikuwa na mamlaka kisheria.

Kuhusu hoja kwamba, upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha pasipo kuacha shaka kesi yao, Jaji Levira amesema upande wa mashtaka ulithibitisha kesi yao.

Baada ya kupitia hoja hiyo, jopo la majaji hao lilitupilia mbali hoja zote zilizowasilishwa na mawakili wa wanandoa hao, hivyo hukumu ya Mahakama Kuu ikabaki kama ilivyoamuliwa dhidi ya wanandoa hao.

Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo, wanandoa hao waliwakilishwa na mawakili watano wakiongozwa na Wakili Jeremiah Mtobesya huku upande wa Jamhuri nao ukiwakilishwa na mawakili watano wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Veronica Matikila.

Licha ya wanandoa hao kushtakiwa kwa pamoja na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela kwa makosa hayo, kila mmoja alikata rufaa kivyake  lakini rufaa hizo zimesikilizwa na kutolewa uamuzi kwa pamoja.

Related Posts