Dar es Salaam. Baada ya kuitumikia Yanga kwa siku 511, kocha Miguel Gamondi leo Novemba 15, 2024 ameonyeshwa mlango wa kutokea kwa kile kinachoonekana ni uongozi wa Yanga kutoridhishwa na mwenendo wa timu msimu huu hasa baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu dhidi ya Azam FC na Yanga hivi karibuni.
Matokeo hayo yameifanya Yanga ijikute ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara na pointi zake 24 huku Simba ikiongoza msimamo wa ligi ikiwa imekusanya pointi 25.
Kumbukumbu zinaonyesha siku 511 ambazo Gamondi ameitumikia Yanga zimekuwa ngumu kwa watani wao wa jadi Simba kutokana na kocha huyo kuiongoza timu yake kutwaa mataji yote muhimu ambayo Simba ilikuwa imepanga kuyatwaa lakini pia kuiwezesha yanga kupata matokeo mazuri kwenye mechi dhidi ya watani wao wa jadi.
Awali ilionekana kama Gamondi angekuwa na wakati mgumu dhidi ya Simba baada ya kupoteza mchezo wa fainali ya Ngao ya Jamii, Agosti 13, 2023 kwa mikwaju ya penalti 3-1 baada ya timu hizo kumaliza dakika 90 za mechi hiyo iliyochezwa katika Uwanja wa Mkwakwani Tanga kwa sare tasa.
Baada ya hapo, Gamondi aliiongoza Yanga kuinyima Simba, mataji mawili makubwa kwenye msimu wa 2023/2024 ambayo ni Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la CRDB na kabla ya kuanza kwa msimu alilipa kisasi kwa kuipora Simba taji la Ngao ya Jamii ambalo ililitwaa mbele yake, mwaka jana.
Mbali na mataji hayo, Gamondi alilipa kisasi cha kufungwa na Simba kwenye Ngao ya Jamii mwaka jana kwa kupata ushindi mara nne mfululizo katika mechi ambazo alikutana nayo kwenye mashindano tofauti.
Vichapo vya Gamondi dhidi ya Simba vilianzia katika ushindi mnono wa mabao 5-1 ambao Yanga iliupata Novemba 4, 2023 katika Ligi Kuu na mechi ya marudiano iliyochezwa Aprili 20, 2024, Simba ikachapwa mabao 2-1.
Timu hizo zilikutana tena katika nusu fainali ya Ngao ya Jamii, Agosti 8 mwaka huu ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0 na zikakutana tena katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu, Oktoba 19, 2024 ambapo Simba ilipoteza kwa bao 1-0.
Sio Simba tu ambayo ilionja ladha ya kuchapwa mabao mengi na Yanga ya Gamondi katika kipindi cha wiki 73 ambacho kocha huyo ameitumikia Yanga.
Ifuatayo ni orodha ya vipigo vikubwa ambavyo Gamondi amewahi kutoa kwa timu mbalimbali katika muda alioifundisha timu hiyo.
Yanga 4-1 Tanzania Prisons
Yanga 5-0 Polisi Tanzania