Meya wa Odessa Gennadiy Trukhanov amesema mashambulizi kwenye mji huo kwa kiasi kikubwa yameharibu majengo, mifumo ya usambazaji wa umeme, makanisa na vituo vya elimu na kukiri kwamba yalikuwa ni mashambulizi makubwa mno kutoka kwa adui.
Kulingana naye, mwanamke mmoja wa miaka 35 aliyekuwa amelala karibu na dirisha ndiye aliyeuawa baada ya jengo la makazi kushambuliwa. Idara za dharura nchini Ukraine zimethibitisha kifo hicho na watu wengine 10 waliojeruhiwa, miongoni mwao, watoto wawili.
Soma pia:Shambulio la Urusi kwenye mji wa Odessa laua mtu 1
Mashambulizi hayo aidha yalisababisha mioto kuwaka kwenye maeneo mbalimbali, lakini ilidhibitiwa mara moja, huku watu wakilazimika kulala kwenye baridi kali kwa kuwa hakukuwa na umeme kutokana na uharibifu uliotokea.
“Jukumu letu hii leo ni kurejesha umeme, kwa sababu mabomba makubwa ya gesi yameharibiwa. Tulisimamisha usambazaji wa umeme na leo mifumo yetu ya dharura inafanya kazi kurejesha nishati hiyo mara moja.” alisema Trukhanov.
Soma pia:Vikosi vya Ukraine vyakabiliana na askari 50,000 wa Urusi katika mkoa wa Kursk
Meya Trukhanov, aliandika kwenye mtandao wa Telegram kwamba zaidi ya watu 40,000 hawakuwa na umeme, lakini jenereta zilikuwa zikifanya kazi kwenye taasisi za tiba.
Akasema ofisi yake ilikuwa ikiwagawia wakazi hao vinywaji vya moto na mablanketi, wakati mabomba ya usambazaji umeme yakiwa yanakarabatiwa.
Soma pia:Urusi yasema iko tayari kwa mazungumzo ya kumaliza vita Ukraine
Orban aitaka EU kufanya mapito mapya ya vikwazo dhidi ya Urusi
Huku hayo yakitokea huko Odesa, Ukraine, Mjini Budapest, Hungary, Waziri Mkuu Viktor Orban ameutolea wito Umoja wa Ulaya kuangazia upya vikwazo dhidi ya Urusi kwa kuwa vinachochea bei kuongezeka na hivyo kuzuia ushindani wa kiuchumi kwenye muungano huo.
Viongozi wa Umoja wa Ulaya walisaini azimio kuhusiana na ushindani kwenye mkutano wao usio wa kawaida wa kilele wiki iliyopita.
Orban amesema kwenye mahojiano na redio moja ya umma nchini humo kwamba bei za nishati zinapaswa kupunguzwa kwa namna yoyote ile, akimaanisha vikwazo dhidi ya Urusi vinapaswa kuangaliwa upya kwa sababu chini ya sera za sasa za vikwazo, bei za nishati hazitashuka.
Orban amekuwa mkosoaji mkubwa wa vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi, tangu taifa hilo lilipomvamia jirani yake Ukraine mapema mwaka 2022, lakini pia amekuwa akiupinga msaada wa kijeshi na fedha wa umoja huo kwa Ukraine.
Wakati mataifa ya Ulaya yakijaribu kwa hali na mali kuacha kutegemea nishati kutoka Urusi, Hungary ambayo haina bandari inapata asilimia 80-85 ya gesi yake kutoka Urusi, na asilimia 80 ya mafuta yake ghafi hutoka kwa mshirika wake huyo wa zamani wa kikomunisti.
Mbali na suala la nishati, taarifa kutoka mjini Berlin zimesema, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz anatarajiwa kujadiliana na Rais Xi Jinping wa China masuala yahusuyo Ukraine na mengineyo.
Berlin imesema wakuu hao wawili watakutana pembezoni mwa mkutano wa viongozi wa kundi la mataifa tajiri na yanayoinukia kiuchumi la G20, Jumanne wiki inayokuja huko Brazil.