Unguja. Kuuziana maeneo bila kushirikisha viongozi wa shehia, kumetajwa kuongeza uvamizi katika maeneo yaliyotengwa na Serikali kwa ajili ya miradi ya jamii.
Changamoto nyingine imetajwa kuwa licha ya maeneo ya wananchi kufanyiwa tathmini na kulipwa fidia wamegoma kuondoka.
Miongoni mwa maeneo hayo ni Maungani, lililoko Mkoa wa Mjini Magharibi ambalo limetengwa kwa ajili ya kuchimba visima ili kukabiliana na tatizo la maji ambalo limevamiwa.
Kutokana na hali hiyo, Wizara ya Maji, Nishati na Madini imesema haitamvumilia mtu yeyote anayejenga katika sehemu iliyohifadhiwa kwa ajili ya kuchimba visiwa vya majisafi na salama. Katika eneo hilo tayari vimechimbwa visima 13.
Akizungumza baada ya kutembelea maeneo hayo leo Novemba 15, 2024, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Joseph Kilangi amesema Serikali imeshafanya tathmini ya maeneo hayo lakini jambo la kushangaza ni kuwa, kuna watu wanauziana viwanja kinyemela hivyo kuongeza uvamizi.
Kilangi amesema licha ya kuwekwa mabango yanayokataza kuendeleza ujenzi katika maeneo hayo, bado wapo wananchi wanapuuza na kuendeleza ujenzi.
“Eneo hili tayari limeshafanyiwa tathmini na waliokuwa wamiliki wake baadhi ya fedha tushawalipa sasa inakuwaje wanauza viwanja,” amehoji.
Amesema wizara haiwezi kuwavumilia watu hao kwa kuwa wanafanya mambo kinyume cha utaratibu wa sheria.
Kilangi amewaomba viongozi wa wilaya na mkoa kuwachukulia hatua watu hao ili iwe fundisho kwa wengine.
Amesema uamuzi wa wizara kwa sasa ni kuwawekea alama za X ili kuwataka wabomoe nyumba zao kupisha ujenzi wa visima vya majisafi na salama kuwezesha kutatua changamoto ya upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
“Kwa sasa uamuzi ni kuendelea kusitisha ujenzi katika maeneo hayo, vyombo vinavyohusika vitekeleze majukumu yao,” amesema.
Sheha wa Shehia ya Maungani, Khamis Bonzo amesema watu wengi wanapojenga au kununua maeneo hawawashirikishi masheha, badala yake huuziana kienyeji.
Kwa mujibu wa Bonzo, awali walikuwa wakisimamisha ujenzi kwa wananchi waliokutwa katika maeneo hayo lakini wanazidiwa na madalali wanaosababisha uvamizi huo.
Othman Ali Othman, aliyeuziwa eneo kinyemela amesema hakujua kuwa maeneo hayo hayaruhusiwi kujengwa ndiyo maana akatoa fedha kununua.
“Sisi hatukujua kuwa maeneo hayo hayaruhusiwi kujengwa ndiyo maana ikafikia hatua hii, kwa hiyo hatuna budi kufuata sheria inavyotaka,” amesema.
Amesema wananchi wengi walionunua maeneo hayo, hawana utamaduni wa kuwashirikisha watu wa ardhi wala masheha, wakiona kwamba wanapoteza muda.
Hivi karibuni akizindua utoaji wa hatimiliki kwa mashamba ya kilimo, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Rahma Kassim Ali alisema uvamizi wa maeneo ndiyo unachochea migogoro ya ardhi Zanzibar.
Hata hivyo, alisema kwa sasa Serikali inakuja na mpango maalumu ambao mtu atakayetaka kununua au kuuza eneo, itamlazimu kutumia mifumo inayoandaliwa itakayopunguza changamoto hiyo.