WAHITIMU VETA LINDI WAOMBA WADAU KUWAWEKEA MAZINGIRA MAZURI YA KUJIARIJI

VIJANA Mkoani Lindi wameiomba serikali na wadau mbalimbali kuendelea kuweka mazingira mazuri ya kuwawezesha kuajiajiri kulingana na fursa zilizopo kama mafuta na gesi ,baada ya kuhitimu vyuo mbalimbali ikiwemo vyuo vya ufundi Stadi ili kupunguza tatizo la ajira.

Ombi hilo limetolewa na wahitimu 188 wa Chuo cha ufundi Stadi Veta Lindi kupitia risala yao waliyoitoa wakati wa mahafali ya 11 ya chuo hicho iliyofanyika Novemba 15,2024.

Vijana hao wamesema kila mwaka chuo hicho kimekuwa kikizalisha wataalam mahiri wenye kuleta ufanisi ambao wakiwekewa mazingira mazuri mbali na kujiajiri wanaouwezo wakuendesha miradi inayosimamiwa na veta,halmashauri na taasisi zingine hivyo kuipunguzia serikali utegemezi wa wataalam hasa mafundi wa kigeni kutoka nje.

Mkuu wa chuo cha Veta Lindi Harry Mmali amesema licha ya chuo hicho kukua tangu kilipoanzishwa mwaka 2012 kwa kuongeza kozi ndefu kutoka fani 5 za awali hadi 12 ikijumuisha ufundi bomba na teknolojia ya majokovu na kiyoyozi lakini pia kozi fupi 21 zinazotolewa kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo,bado kuna mwamko mdogo wa vijana kujiunga na chuo hicho.

Amewaomba wadau mbalimbali kushirikiana na chuo hicho katika kuihamasisha jamii ili kutambua umuhimu wa mafunzo hayo katika ujenzi wa uchumi wa nchi hasa fursa za uwepo wa gesi asilia kwa Mkoa wa Lindi.

Kwa upande wake,Juma Namuna ,Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii NSSF Mkoani Lindi ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo amewakumbusha vijana kutumia ujuzi waliopata kuleta maendeleo kwa kufanya kazi kwa weledi na uaminifu mkubwa wakijiunga katika vikundi waweze kupata mikopo itakayowawezesha kujiajiri huku akitaka chuo kiimarishe mahusiano na makampuni na viwanda ili mafunzo wanayotoa yakidhi mahitaji ya soko la ajira.




Related Posts