Waandamanaji hao walizitaka nchi tajiri, ambazo zinahusika na uzalishaji mkubwa wa gesi chafuzi zinazochangia ongezeko la joto duniani, kulipia kiwango kinachostahili katika mazungumzo ya ufadhili wa hali ya hewa yanayoendelea mjini Baku.
Mmoja wa wanaharakati hao wa mazingira Amalen Sathananthar ametoa wito wa mabadiliko ya haki, ya usawa, na yanayofadhiliwa kuachana na matumizi ya nishati ya visukuku na badala yake kugeukia matumizi ya nishati jadidifu.
Wanaharakati wanataka ufadhili zaidi kwa mataifa ya Afrika
Baadaye, wanaharakati wa mazingira kutoka Afrika, walifanya maandamano wakitaka ufadhili zaidi kuzisaidia nchi za Afrika kukabiliana na athari ya mabadiliko ya tabianchi.
Mwanaharakati Afanyu Yembe Njamnshi amesema wanahitaji kuongeza mara dufu kiasi cha fedha zinazopelekwa Afrika kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuwepo kwa ruzuku zaidi badala ya uwekezaji au mikopo .
Zaidi ya wadau 1,700 wa nishati ya mafuta ya visukuku wanahudhuria mkutano wa COP29
Muungano wa mashirika yasio ya kiserikali unaojulikana kama ”Kick the Big Polluters Out” KBPO umechambua uidhinishaji wa kuhudhuria kongamano hilo la kila mwaka la tabia nchi, na kubainisha kuwa zaidi ya watu 1,700 wanaohusishwa na nishati ya mafuta ya visukuku wanahudhuria.
David Tong kutoka kundi la wanaharakati la Oil Change International, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba hali hiyo ni kama kuwepo kwa wanaharakati wa matumizi ya tumbaku katika kongamano la Saratani ya mapafu.
Tofauti zaibuka katika mkutano wa COP29
Hapo jana, makamu wa rais wa zamani wa Marekani na mwanaharakati mkuu wa hali ya hewa Al Gore, alisema inasikitisha kwamba sekta ya nishati ya visukuku na mataifa ambayo uchumi wake unategemea zaidi uchimbaji na usafirishaji wa mafuta au gesi asilia zimechukuwa udhibiti wa mchakato wa COP kwa kiwango kisichofaa.
Mikutano ya COP haitimizi majukumu yake
Kundi la wanaharakati wakuu wa hali ya hewa na wanasayansi wameonya leo kwamba mchakato waCOP hautekelezi tena majukumu yake.
Katika barua iliyotiwa saini na wanaharakati mbalimbali akiwemo katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, wamehimiza kuwepo kwa mikutano midogo ya mara kwa mara yenye uwajibikaji mkubwa pamoja na vigezo vikali kwa nchi zitakazokuwa wenyeji wa mikutano hiyo.
COP29: Mataifa masikini yapewe fedha zaidi
Pia walitoa wito wa sheria za kuhakikisha kampuni zinaonyesha kujitolea wazi kwa masuala ya hali ya hewa kabla ya kuruhusiwa kutuma wawakilishi kwenye mazungumzo hayo.