Wawili Benki ya NBC kortini madai ya wizi , kutakatisha Sh390 milioni

Dar es Salaam. Wafanyakazi Wawili wa Benki ya NBC, Johnson Kato (57) na Gasper Kimaro (30) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka sita yakiwemo ya kujipatia Sh390 milion kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha hizo.

Washtakiwa hao wanadaiwa kujipatia fedha hizo, mali ya Mfuko wa Dhamana ya Maendeleo ya Jamii Tanzania (CDTF), baada ya kughushi hundi mbili na kudai kuwa zimesainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko, wakati wakijua si kweli.

Kato ambaye ni mkazi wa Mbezi Beach  na Kimaro ambaye ni mkazi wa Vijibweni Kigamboni, wamesomewa mashtaka yao leo Novemba 15, 2024 na wakili wa Serikali Frank Rimoy, mbele ye Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki.

Wakili Rimoy alidai kuwa washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 32474/2024.

Kati ya mashtaka sita yanayowakabili, mawili ni ya kughushi hundi, mawili ya kutakatisha fedha, mawili ya kujipatia fedha hizo kwa njia ya udanganyifu.

Hata hivyo, kabla ya washtakiwa kusomewa mashtaka yao, Hakimu Nyaki aliwaeleza washtakiwa hao kuwa kesi inayowakabili mbele yao ni ya uhujumu uchumi ambayo mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza labda kwa kibali maalumu.

Pia mashtaka ya kutakatisha fedha yanayowakabili washtakiwa hao, hayana dhamana kwa mujibu wa sheria hiyo wataendelea kusalia mahabusu.

Mahakama kutoa maelezo hayo, washtakiwa hao waliokuwa wamevalia nguo nyeusi, waliinamisha vichwa chini.

Baada ya maelezo hayo, Wakili Rimoy aliwasomea mashtaka yao, ambapo shtaka la kwanza ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kinyume na kifungu 301 na 302 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa Oktoba 23, 2023 katika Benki ya NBC, tawi la Cooperate wilaya ya Ilala, wakiwa kama wafanyakazi wa benki hiyo, kwa nia ya kutapeli walijipatia Sh195 milioni kutoka katika akaunti namba 011103003058 kwa kutumia hundi yenye namba 004459, wakionyesha kuwa hundi hiyo imetolewa na kusainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Dhamana ya Maendeleo ya Jamii Tanzania (CDTF), wakati wakijua si kweli.

Shtaka la pili, siku na eneo hilo kwani ya kutapeli, walinipatia Sh195 milioni kutoka katika akaunti hiyo kwa kutumia hundi yenye namba 004460, wakionyesha kuwa hundi hiyo imetolewa na kusainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Dhamana ya Maendeleo ya Jamii Tanzania (CDTF), wakati wakijua si kweli.

Shitaka la tatu na la nne ni kughushi hundi hizo, tukio wanalodaiwa kulitenda siku na eneo hilo.

Washakiwa hao wanadaiwa kughushi hundi yenye namba 004459 na 004460 wakionyesha hundi hiyo zimetolewa na kusainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Dhamana ya Maendeleo ya Jamii Tanzania (CDTF), wakati wakijua si kweli.

Rimoy alidai katika shtaka la tano na la sita ni kutakatisha fedha, ambapo washtakiwa kwa pamoja katika tarehe hiyo na  eneo hilo, wakiwa wafanyakazi wa benki hiyo, walijipatia jumla ya Sh390 milioni kupitia hundi mbili tofauti, wakati wakijua fedha hizo ni kosa la uhalifu wa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kusajili nyaraka muhimu mahakamani hapo.

Pia waliomba wapewe tarehe nyingine ili wawasilishe kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) cha kuruhusu Mahakama hiyo kusikiliza shauri hilo.

Hakimu Nyaki baada ya kusikiliza maelezo hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 28, 2024.

Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana mashtaka ya kutakatisha fedha hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

Related Posts