Wanakutana kabla ya mkutano wa ana kwa ana chini ya wingu la utata wa kidiplomasia kati ya Beijing na Washington uliotokana na ushindi wa Donald Trump katika uchaguzi wa Marekani.
Xi na Biden waliwasili Lima jana Alhamisi pamoja na viongozi wengine wa dunia kwa mkutano wa siku mbili wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya ushirikiano wa kiuchumi wa nchi za Asia-Pasifiki, kujadili biashara na uwekezaji kwa kile kinachotajwa kama ukuaji jumuishi.
Viongozi hao wa China na Mareknai wanatarajiwa kufanya mazungumzo kesho Jumamosi, katika kile afisa wa utawala wa Marekani alisema pengine utakuwa mkutano wa mwisho kati ya Xi na Biden kabla ya Trump kuapishwa rasmi mnamo mwezi Januari.
Soma pia: China na Marekani zakubaliana kuanza tena mazungumzo ya ngazi za juu ya kijeshi
Mahusiano ya kidiplomasia kati ya mataifa hayo yenye uchumi mkubwa duniani yako katika mizani wakati rais mteule wa Marekani Donald Trump akiwa ameashiria uwezekano wa kukabiliana na Beijing katika muhula wake wa pili, hatua inayosababisha mkutano kati ya viongozi hao kufuatiliwa kwa karibu.
Lakini kutokuwa na uhakika juu ya hatua zinazofuata za Trump sasa kunafunika ajenda ya mkutano huo, kama inavyofanyika katika mkutano wa COP29 unaoendelea Azerbaijan, pamoja na mkutano wa kilele wa G20 utakaoandaliwa Rio de Janeiro wiki ijayo.
Soma pia: APEC kuzingatia zaidi masuala ya usawa na mazingira
China yazidi kujiimarisha
China ni mshirika wa Urusi na Korea Kaskazini, na inajenga uwezo wake wa kijeshi huku ikizidisha shinikizo kwa Taiwan, ambayo inadai kuwa sehemu ya eneo lake. Pia inapanua ufikiaji wake katika Amerika ya Kusini kupitia miundombinu na miradi mingine chini ya Mpango wake wa ujenzi wa miundombinu ya treni na barabara wa Belt na Road.
Akizungumza baada ya uzindizi wa daraja lililofadhiliwa na China mwenyeji wa mkutano wa APEC, Rais wa Peru, Dina Boluarte amesema:
“Kwa mradi huu mkubwa tunaanza mabadiliko ambayo yataimarisha nchi kama kitovu cha kimataifa cha usafirishaji, kiteknolojia na kiviwanda ambacho kitatuimarisha katika eneo la Asia Pacific.”
Mkutano huo pia utahudhuriwa na viongozi wa Japan, Korea Kusini, Canada, Australia na Indonesia, miongoni mwa mataifa mengine japo Rais Vladimir Putin ambaye pia ni mwanachama wa APEC hatokuwepo.
Jumuiya ya APEC, iliyoundwa mwaka wa 1989 kwa lengo la kukuza biashara huria ya kikanda, inazijumuisha nchi 21 ambazo kwa pamoja uchumi wake unawakilisha takriban asilimia 60 ya pato la taifa la dunia na zaidi ya asilimia 40 ya biashara ya kimataifa.