IKIWA imesalia takribani mwezi mmoja kabla ya dirisha dogo la usajili kufunguliwa Desemba 15 mwaka huu, Yanga SC imerusha ndoano kuwania saini ya beki wa kati wa Coastal Union, Lameck Lawi ambaye awali alikuwa kwenye rada za Simba kabla ya mvutano kutokea na kila mmoja kwenda na njia yake.
Uamuzi huo wa Yanga ambao inaelezwa uko kwenye hatua nzuri za awali, umekuja baada ya changamoto walizozipata kwenye safu ya ulinzi kutokana na upungufu wa mabeki wa kati walipocheza mechi ya ligi dhidi ya Tabora United, ambapo walilazimika kuwatumia viungo Khalid Aucho na Aziz Andabwile.
Ilikuwaje? Kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Tabora United uliochezwa Novemba 7 mwaka huu ambao Yanga ilipoteza kwa mabao 3-1, walikosa huduma ya mabeki wao wawili wa kati, Ibrahim Hamad ‘Bacca’ na Dickson Job, hivyo walilazimika kumtumia kiungo mkabaji, Andabwile kucheza sambamba na nahodha Bakari Mwamnyeto.
Dakika kumi baada ya mchezo huo kuanza, Andabwile aliumia, hivyo Yanga ikalazimika kumtumia kiungo Khalid Aucho kama beki wa kati ambaye alicheza sambamba na Mwamnyeto, hali iliyodhihirisha upungufu kwenye ulinzi.
Lawi ambaye awali alikuwa akihusishwa na Simba katika kipindi cha dirisha kubwa la usajili la kuingia msimu huu ambao ulikwama, anajulikana kwa uwezo wake wa kucheza kama beki wa kati anayetumia vizuri zaidi mguu wa kushoto.
Beki huyo mshindi wa tuzo ya mchezaji bora kijana wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2022-23, ameibuka kuwa moja ya wachezaji wanaowindwa na Yanga kwa lengo la kuongeza nguvu kwenye ulinzi wa timu hiyo.
Mbali na umri wake mdogo wa miaka 19 alionao ambao unatoa msingi wa uwekezaji wa muda mrefu, Yanga inaona fursa ya kujenga safu ya ulinzi imara na ya kuaminika kwa kuongeza mchanganyiko wa mabeki wa miguu tofauti, hali itakayosaidia kuleta uthabiti zaidi katika kikosi hicho.
Lawi ni mchezaji mzawa mwenye sifa zinazofaa kwa malengo ya muda mrefu ndani ya Yanga. Kwanza, ni kijana mwenye umri mdogo ambaye anaweza kuchukua nafasi ya uongozi kwenye safu ya ulinzi kwa miaka mingi ijayo. Aidha, Lawi ni beki wa kati anayetumia mguu wa kushoto, jambo ambalo ni faida kwa timu kuwa na mtu wa aina hiyo eneo la ulinzi wa kati.
Faida ya kuwa na beki wa kati anayetumia mguu wa kushoto inaifanya timu kuwa na balansi nzuri upande wa ulinzi wa kushoto ambapo beki huyo anasaidiana na yule wa pembeni vizuri kulinganisha na beki wa kati anayetumia mguu wa kulia.
Timu nyingi zimekuwa na mabeki wa kati ambao wote wanatumia mguu wa kulia ambapo mara kadhaa upande wa kushoto unakuwa na udhaifu na wapinzani kuutumia sana kupeleka mashambulizi.
Ukiangalia pale England, Arsenal mabeki wao wa kati, Gabriel Magalhaes anatumia mguu wa kushoto wakati William Saliba akitumia kulia, lakini pia hata Manchester United, kuna Lisandro Martinez anayetumia mguu wa kushoto akicheza beki wa kati.
Ukiangalia katika upangaji wa timu, beki wa kati anayetumia mguu wa kushoto hupangwa upande huohuo kuongeza nguvu kwa beki wa kushoto wakati mwenzake akiwekwa upande ambao ataongeza nguvu kulia.
Katika soka la Tanzania, ni adimu kuliona hilo kitu ambacho timu zinazohitaji balansi kwenye eneo la ulinzi zimekuwa zikihitaji mabeki wa aina ya Lawi.
Kwa sasa pale Yanga, Ibrahim Bacca ambaye ana uwezo wa kutumia mguu wa kushoto licha ya kwamba kiuhalisia mguu anaoutumia zaidi ni wa kulia, ndiye anayetumika kucheza upande wa kushoto kumsaidia Nickson Kibabage au Chadrack Boka. Pale Simba, Abdulrazack Hamza pia ana uwezo wa kutumia mguu wa kushoto.
Kitendo cha Yanga kumpigia hesabu Lawi, inaweza kusaidia sana kuongeza uwiano kwenye safu ya ulinzi ya timu hiyo ambayo kwa sasa inajumuisha mabeki wa kati wanaotumia miguu ya kulia.
Uwepo wa Lawi katika kikosi unaweza kuongeza usawa wa kimfumo na kuimarisha utulivu wa kikosi katika kukabiliana na mashambulizi ya wapinzani wenye mbinu tofauti.
Mbali na hilo, mafanikio ya Bakari Mwamnyeto ambaye alitua Yanga mwaka 2020 akitokea Coastal Union, inawapa matumaini Yanga kuwa Lawi atafuata nyayo za nahodha huyo aliyeshinda mataji matatu mfululizo ya Ligi Kuu Bara na Kombe la FA.
Katibu Mkuu wa Coastal Union, Ayoub Omary, ameweka wazi klabu yake iko tayari kufanya biashara na Yanga endapo watawasilisha rasmi ofa yenye kuvutia na inayokidhi thamani ya Lawi.
Omary alibainisha kuwa Yanga inakaribishwa kwa mazungumzo rasmi, lakini pia alisisitiza kuwa Coastal inathamini sana mchango wa Lawi kwenye timu hiyo na kwamba wangependa kuona thamani yake inazingatiwa kwenye ofa yoyote itakayowasilishwa.
“Lawi ni beki kijana lakini amekuwa na mchango mkubwa kwa Coastal Union, na pia amesaidia sana timu ya taifa ya vijana, Ngorongoro Heroes kufuzu kwa michuano ya AFCON U20 ya mwaka 2025. Yanga na klabu nyingine yoyote inakaribishwa mezani kama kweli wanamuhitaji, “ alisema Omary.
Kwa Yanga, usajili wa Lawi ni sehemu ya mpango mpana wa kuongeza vipaji vya ndani vyenye uwezo wa kipekee na gharama nafuu.
Wakiwa wanapambana katika michuano ya ndani na ile ya kimataifa, Yanga wanaamini kuwa uwepo wa Lawi unaweza kusaidia kuziba mapengo yaliyopo na kupunguza utegemezi mkubwa kwa mabeki wa kimataifa.
Lawi anatarajiwa kuwa suluhisho la muda mrefu linaloweza kuleta mbinu tofauti za ulinzi na kuleta nguvu zaidi katika safu ya ulinzi.
Mashabiki wa Yanga wanasubiri kwa hamu kuona mchakato wa usajili ukikamilika, ikizingatiwa timu hiyo ya Jangwani imefungiwa kusajili na FIFA kutokana na kushindwa kesi ya mchezaji wake wa zamani Augustine Okrah, ambaye ilimuacha bila ya utaratibu.
Ikiwa usajili huu utafanikishwa, Yanga itakuwa imejiweka katika nafasi nzuri ya kumudu changamoto kwa kuwa na kikosi imara, kilichojaa vipaji chipukizi na wazoefu.
Hata hivyo, ujio wa Lawi ndani ya Yanga hautasababisha mchezaji yeyote kukatwa kwani hadi sasa kikosi hicho kina nyota 27 waliosajiliwa wakiwa na gepu la kuongeza wazawa watatu baada ya kutimiza idadi ya nyota 12 wa kimataifa kikanuni.
Taarifa ya Simba iliyotolewa Juni 20 mwaka huu, ilisomeka hivi; “Klabu ya Simba imefanikiwa kumsajili mlinzi wa kati Lameck Elius Lawi kwa mkataba wa miaka mitatu kukiwa na kipengele cha kuongeza mwaka mmoja akitokea Coastal Union ya Tanga.
“Lawi ni kijana mwenye kipaji kikubwa na amekuwa ngome imara kwenye kikosi cha Coastal msimu uliopita na hicho ndicho kilichotuvutia kumsajili.
“Usajili wa Lawi ni mkakati wa kuijenga Simba mpya yenye ushindani kuelekea msimu wa mashindano wa 2024/25.
“Lawi mwenye umri wa miaka 18 na umbile refu anakuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa katika kikosi chetu kuelekea msimu mpya wa Ligi.
“Lameck Lawi licha ya umri wake mdogo lakini ni mlinzi mwenye uwezo mkubwa aliyewavutia wapenzi wa mpira nchini Tanzania na nje ya mipaka ya nchi yetu na usajili wake tunategemea ataongeza kitu kikubwa katika kikosi akisaidiana na walinzi wazoefu waliokuwepo.”
Hata hivyo, Lawi hakuitumukia Simba baada ya Wagosi wa Kaya kuibuka na kudai wekundu hao wa Msimbazi walishindwa kufuata makubaliano ya kimkataba.
Ni yapi hayo? Inaelezwa kwamba ni juu ya pesa za usajili ambazo zilitakiwa kuingizwa zote kabla ya Mei 30 mwaka huu.
Simba walihitaji wamlipe Sh5 milioni kwa kila mwezi kama mshahara wake wa mkataba, lakini baada ya kuchelewa kufanya malipo ya uhamisho wa mchezaji huyo kutoka Coastal Union, ikaibuka timu nyingine kutoka Ubelgiji, Gent, ambayo ilitaka kumlipa mchezaji huyo Sh25 milioni kwa mwezi.
Baada ya Coastal Union kuona mzigo wa maana ilibadili mwelekeo na kuamua kurejesha fedha ambazo Simba waliweka kwenye akaunti nusu ya makubaliano Sh100 milioni badala ya Sh230 milioni.
Sakata hilo lilizifanya Simba na Coastal kufikishana Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji huku mchezaji huyo akiwa zake Ubelgiji ambako napo mambo hayakumwendea vizuri ikabidi kurejea Tanzania, akakuta suala lake limemalizika huku akiidhinishwa kuendelea kutumika kwa Wagosi wa Kaya hao.