ACT-Wazalendo yataka Waziri Mchengerwa kufuatilia agizo lake la rufaa

Dar es Salaam. Chama cha ACT-Wazalendo, kimedai kuwa utekelezaji wa kupitia rufaa za wagombea walioenguliwa,  haujafanywa kwa ufanisi licha ya maelekezo ya Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa.

Novemba 12,2024 Waziri Mchengerwa aliongeza muda wa uwasilishaji wa rufaa hadi jana Ijumaa Novemba 15, saa 12 jioni, akizitaka kamati  za wilaya kuitisha fomu za wagombea wote

Hatua hiyo ilitokana na malalamiko ya vyama vya upinzani ya wagombea wao kuenguliwa, jambo lililosababisha CCM kupitia katibu mkuu wa chama hicho, Dk Emmanuel Nchimbi kuiomba Tamisemi kuyapuuza makosa madogo yaliyojitokeza wakati kwa wagombea wakati wa ujazaji wa fomu, ili kuwepo wagombea wengi katika uchaguzi huo.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari leo Jumamosi Novemba 16, 2024, Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo (bara), Isihaka Mchinjita amesema chama hicho, kimefuatilia kwa karibu na kufanya tathmini ya kina kuhusu mwenendo wa mchakato huo na kujiridhisha hakuna kilichofanyika.

“Mathalani, wagombea wetu wote katika majimbo ya Tandahimba (500), Newala Vijijini (93), Kinondoni (80) na Bukoba Vijijini (621), wameendelea kuenguliwa na kamati za rufaa. Hali ni hiyohiyo kwenye takriban majimbo mengi yaliyopokea majibu ya rufaa.

“Kwenye halmashauri nyingi, wasimamizi wa uchaguzi hawajaitisha fomu za uteuzi ili kufanya mapitio ya kuwarejesha wagombea walioenguliwa kwa masuala ya udhamini wa chama, kama ilivyoagizwa na Waziri Mchengerwa,” amesema.

Mchinjita amesema ACT- Wazalendo imesikitishwa na kitendo cha kamati za rufaa kuendelea kuwaengua wagombea wao vijiji, mitaa na vitongoji takribani wote waliokata rufaa.

“ACT- Wazalendo tunajiuliza inawezekanaje kwa wasimamizi wa uchaguzi na kamati za rufaa kupuuza maelekezo ya kuwarejesha wagombea walioenguliwa ambayo Katibu Mkuu wa CCM, Dk Nchimbi alisema yametoka kwa Rais wa Samia Suluhu Hassan,” amesema Mchinjita.

Kutokana na mwenendo huo, ACT-Wazalendo inataka Waziri Mchengerewa kufuatilia kwa umakini utekelezaji wa agizo lake kwa kamati za rufaa na wasimamizi wa uchaguzi, ili kutenda haki na kuwarejesha wagombea.

“ACT-Wazalendo itamwandikia barua Waziri wa Tamisemi (Mchengerwa), kumweleza  maeneo ambayo agizo lake halijatekelezwa pamoja na vielelezo ili achukue hatua.

“Tutafungua kesi mahakamani kupinga kuenguliwa kwa wagombea wetu ili kuhakikisha uchaguzi unarudiwa tena, wanasheria wote wa chama   wameagizwa kujiandaa kufungua kesi kwenye vijiji, mitaa na vitongoji vyote,” amesema Mchinjita.

Mbali na hilo, Mchjinjita amesema chama hicho, kitawasilisha maombi kwa Chama cha Wanasheria Tanzania Tanganyika (TLS) kuomba msaada mawakili zaidi wa kutekeleza mchakato huo wa kufungua kesi.

Katika hatua nyingine, Mchinjita amesema ACT-Wazalendo kitaendelea na kampeni kabambe kwenye maeneo ambayo wagombea wao wameteuliwa.

“Chama kimejiandaa kwa kampeni ya kishindo na za kisayansi kuhakikisha kinapata ushindi kwenye mitaa, vijiji na vitongoji vyote ambavyo tuna wagombea,” amesema Mchinjita.

Kwa mujibu wa Mchinjita, kesho Jumapili Novemba 17, 2024, ACT – Wazalendo kitazindua ilani ya uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji itakayotoa mwongozo wa kisera kwa wagombea wa chama hicho.

Related Posts