Arusha. Harufu kali mithili ya mzoga wa mnyama iliyotoka ndani ya nyumba ya John Lema (57), mkazi wa Mtaa wa Sokoni II jijini Arusha, imesaidia jamii inayozunguka nyumba yake kufichua kifo chake ambacho chanzo chake bado hakijajulikana.
Inasadikika Lema amekufa siku nne zilizopita akiwa ndani ya nyumba yake ambayo anaishi peke yake, hivyo mwili wake ulivimba na kuanza kuoza bila kugundulika hadi kutoa harufu kali iliyowashtua majirani zake.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, leo Novemba 16, 2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Justine Masejo amesema walipata taarifa kuhusu kifo hicho Novemba 14, 2024 na askari walifika eneo la tukio wakauchukua mwili wa marehemu.
“Mwili umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya Rufaa Mount Meru kwa uchunguzi na upelelezi zaidi utakapokamilika utakabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya taratibu zingine,” amesema Kamanda Masejo.
Wakizungumza eneo la tukio, mjumbe wa Mtaa wa Sokoni II, Lucas Mollel amesema amegundua kifo cha marehemu baada ya kupita pembeni ya nyumba yake na kusikia harufu kali mithili ya mzoga na alipojaribu kuita bila majibu, akaamua kutoa taarifa kwa ndugu zake.
“Asubuhi nilipita hapa nikasikia harufu lakini sikutilia maanani lakini kadri muda unavyokwenda, harufu ilizidi, nikaamua kumuita, sikujibiwa. Nilipotafuta upenyo wa kuchungulia, sikufanikiwa ndio nikaamua kwenda kwa kaka yake na kumkuta mke wake, ndipo tukaja naye na majirani wachache tukaanza kubomoa geti,” amesema na kuongeza:
“Tulifanikiwa kubomoa geti lake lililokuwa limefungwa kwa ndani kwa kufuli na kukuta ndani mlango uko wazi ndio tukaingia na kukuta kweli jirani yangu amefariki akiwa amekaa kwenye kiti huku mwili ukiwa umevimba na umeanza kuoza, ndipo tukaita polisi kuja kuchukua mwili.”
Mke wa kaka wa marehemu, Judith Munisi amesema marehemu shemeji yake huwa anaishi peke yake baada ya kufukuza wapangaji wote kwenye nyumba yake tangu mwanzoni mwa mwaka huu na kuamua kuishi peke yake. Marehemu hajawahi kuoa wala kuwa na mtoto.
“Shemeji yangu huwa anaishi peke yake baada ya kushindwana na wapangaji wake aliokuwa anaishi nao hapa na sijawahi kusikia akiwa anaumwa chochote zaidi ya leo kuambiwa hajaonekana tangu Jumatatu na kuna harufu ndani kwake. Tumekuja tukabomoa geti na kukuta kweli amefariki hapa akiwa amekaa na mwili umeanza kuoza,” amesema.
Kwa upande wake, mkazi wa eneo hilo, Joel Lazaro amesema kuwa mwili wa Lema ulianza kuharibika kutokana na kukaa muda mrefu. Amewashauri watu waliofikia umri wa kuoa au kuolewa kuishi na wenza ili kuepuka matatizo kama hayo kutokea.
“Maisha haya lazima tuishi kama taasisi, kuishi peke yako matatizo kama haya ndio yanatokea maana si ajabu hata Lema aliumwa lakini akakosa msaada au kama siku zake zilifika asingeoza hivi, lazima angesaidiwa na kuhifadhiwa kwa taratibu na heshima kabla ya kuharibika,” amesema.