Dah! Gamondi aondoka na utamu wake, rekodi zake ziko hivi

YANGA imeachana na kocha Gamondi na Moussa Ndaw rasmi. Sehemu ya taarifa iliyotolewa ilisema; “Uongozi wa Young Africans Sports Club unapenda kuutarifu umma kuwa umevunja mkataba na Kocha Mkuu wa kikosi cha kwanza, Angel Miguel Gamondi. Vilevile, Uongozi wa Young Africans Sports Club, umesitisha mkataba wa kocha msaidizi wa kikosi cha kwanza, Moussa Ndaw.”

Gamondi alijiunga na Yanga Juni 24, 2023 akichukua nafasi ya Mtunisia Nasreddine Nabi aliyeipa mataji mawili ya Ligi Kuu, mawili ya Kombe la Shirikisho (ASFC), mawili ya Ngao ya Jamii na kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Tangu ateuliwe kukiongoza kikosi hicho, Gamondi amekiongoza katika jumla ya michezo 40 ya Ligi Kuu Bara kuanzia msimu wa 2023-2024, hadi huu wa sasa wa 2024-2025, ambapo kiujumla kati ya hiyo ameshinda 34, sare minne na kupoteza pia minne.

Katika michezo hiyo 40 ya msimu uliopita na huu wa sasa, safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho cha Gamondi imefunga jumla ya mabao 85 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 18, ambapo kiujumla kwa misimu miwili amekusanya pointi zake 104.

Gamondi amechukua mataji matatu na timu hiyo akianza na Ligi Kuu Bara msimu uliopita na kukifanya kikosi hicho kufikisha jumla ya mataji 30, tangu mwaka 1965, akachukua pia Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Ngao ya Jamii kwa msimu huu. Gamondi aliipeleka timu hiyo hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza baada ya miaka 25, kufuatia kufanya hivyo mara ya mwisho 1998.

Ushindi wa mabao 4-0, ilioupata Yanga dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria Februari 24, 2024, katika hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, ulimfanya Gamondi kuandika rekodi mpya ya kuivusha robo fainali kwa mara ya kwanza kwenye historia yao.

Gamondi aliandika rekodi nyingine mpya ya kibabe kwa kuifanya Yanga iwe ya kwanza nchini kushinda mabao mengi zaidi kwa timu za Kaskazini.

Ushindi huo wa mabao 4-0, dhidi ya CR Belouizdad uliifanya kuivuka rekodi iliyokuwa inashikiliwa na Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2018-2019 ambapo ilikuwa ya kwanza nchini kuifunga JS Saoura ya Algeria kichapo cha mabao 3-0.

Moja ya jambo kubwa litakalokumbukwa kwa Gamondi ni kuiwezesha timu hiyo kushinda kwa mabao 5-1, dhidi ya Simba Novemba 5, 2023, yaliyofungwa na mastaa, Kennedy Musonda, Stephane Aziz KI na Pacome Zouzoua huku Maxi Nzengeli akifunga mawili.

Simba ilikuwa haijawahi kufungwa na Yanga idadi kama hiyo kubwa ya mabao tangu ilipolazwa 5-0 mwaka 1968, kipigo ambacho Simba ilikilipa kwa kishindo mwaka 1977 kwa kuifumua Yanga 6-0 kisha kupigilia msumari mwingine wa mabao 5-0 mwaka 2012.

Kichapo hicho kilimfukuzisha kazi Kocha Mbrazili, Roberto Oliveira ‘Robertinho’, ambaye alikuwa na rekodi nzuri mbele ya Yanga akiifunga mara tatu kwenye mechi tofauti ikiwemo ya Ligi Kuu Bara na Ngao ya Jamii, japo mambo yote yalibadilika.

Tangu aingie madarakani kuiongoza timu hiyo, Gamondi amesajili nyota wapya 18 kutoka klabu mbalimbali.

KILICHOMTOA GAMONDI YANGA

Yanga imembebesha lawama zote Miguel Gamondi ambaye anaonekana kama falsafa zake zimeshakuwa kitu rahisi kukamatika kwa wapinzani wao. Hizi ni baadhi ya changamoto zilizompotezea kazi.

Makosa ya kiufundi ambayo kocha huyo ameyaonyesha yakiwemo namna ambavyo ameshindwa kutengeneza timu inayolingana kiushindani baina ya wachezaji, ni kati ya mambo yalimpotezea sifa.

Wachambuzi wa mambo wanasema ukitazama namna mtangulizi wake Nasreddine Nabi alitengeneza kikosi kilichokuwa na ushindani sahihi wa nafasi za wachezaji, ilikuwa ngumu kuona tofauti kubwa anapocheza Kibwana Shomari dhidi ya Djuma Shaban, au hata anapocheza Zawadi Mauya au Khalid Aucho.

Hili limeshindwa kuwa endelevu kwa Gamondi ambaye ni kama alikuwa na kundi moja tu la wachezaji anaowaamini ambao nje yao inaonekana ni ngumu kupenya na kuisaidia tena timu hiyo.

Sio jambo la kujificha kwamba nidhamu kwa baadhi ya wachezaji wa Yanga ilishuka, hata uwe na msuli gani wa utetezi huwezi kupinga namna wachezaji wa Yanga wanavyozagaa wakifanya starehe hatarishi ndani ya msimu.

Mbaya zaidi wachezaji hao wameshindwa kutunza hadhi yao kwa kujiachia wakirekodiwa na kwa nyakati kama hizi video za namna hiyo hata kama starehe hizo zitakuwa zilifanyika katika nyakati zilizostahili, hakuna ambaye anaweza kuwaelewa.

Gamondi alikuwa anaiingiza timu yake kambini siku moja kabla ya mchezo yaani Yanga iliingia kambini Jumatano kisha ikaenda kucheza na Tabora United Alhamisi, ikitokea wachezaji wakashindwa kujilinda sawasawa huko mtaani ni vigumu kocha kueleweka.

Achana na kikosi cha Yanga, angalia mashabiki wao na hata baadhi ya viongozi baadhi yao walionyesha kama timu yao ni vigumu kufungika tena, hali ilikuwa kama wameshindikana, wakajisahau kwamba kuna timu zinaumiza vichwa kwamba watawezaje kuwazuia.

Ndani ya Yanga kuanzia mashabiki, viongozi mpaka wachezaji wanatakiwa kubadilika wakitambua kwamba hata uwe bora namna gani, unaweza kufungika kama utashindwa kutunza ubora wako kwa kuridhika.

Wengi ndani ya Yanga wakiona kikosini wana watu kama Clatous Chama, Pacome Zouzoua, kule Stephanie Aziz KI mara huku yupo Ibrahim Bacca basi kazi imekwisha, wanasahau kwamba ndege mjanja hunaswa tundu bovu.

Wachezaji wa Yanga wanatakiwa kuambiwa ukweli zaidi na zaidi kwamba majina yao hayatashinda mechi bali kwa kuzingatia nidhamu ya mchezo na pia kwamba viongozi wa klabu hiyo walisajili vipaji vyao na sio ukubwa wa majina yao.

Kubomoka kwa nidhamu ya wachezaji wa Yanga, wengi watawalaumu nyota wao, lakini kuna hawa wapambe ambao sasa wanaitwa ‘chawa’. Uongozi wa klabu hiyo ni lazima uwatazame chawa hawa kwa jicho la ukali kwani wana ushawishi mbaya kwa wachezaji.

Ukizunguka usiku unakutana nao wako na wachezaji wao, kukicha utawaona wako na viongozi wao, likishaibuka balaa kama hili haraka wanakaa upande wa viongozi.

Kundi hili ni hatarishi zaidi, linajua kuunganisha watu na kisha kukaa pembeni wanasubiri anguko ili kisha wauwashe moto. Nani anatakiwa kuokoa jahazi ni viongozi wenyewe kwa kuwaambia ukweli wachezaji wao kwamba wanaokaa nao na kufanya nao starehe ndio haohao watasambaza mambo yao endapo watakosa kujitambua kufanya mambo yao bila ya weledi.

Yanga wanatakiwa kutambua ligi ni ngumu na kila timu inautaka ubingwa, watani wao wamebadilika, wamefanya usajili mkubwa na kiufupi kila timu imejipanga kwa hesabu zake, hivyo haitakuwa rahisi kwao kutetea ubingwa endapo wataendelea kujiona kama wao ndio bora kuliko wengine.

Related Posts