Dk Mpango ataka uimarishwaji vituo vya ufuatiliaji kaboni, rasilimali kijani

Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema ni muhimu kwa nchi za Afrika kuimarisha vituo vyake vya ufuatiliaji wa hewa ya kaboni,  ili kuweza kunufaika na biashara yake ambayo sasa imefikia thamani ya Dola za Marekani 900 bilioni katika soko la dunia.

Dk Mpango amesema nchi za Afrika zinapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuchochea mijadala kwenye jumuiya za kimataifa ili  kutambua umuhimu wa rasilimali kijani kuwa sehemu ya pato la Taifa kwa mataifa ya Afrika.

Amesema hayo wakati wa mkutano wa wakuu wa nchi na serikali kuhusu utajiri wa kijani kwa mataifa ya Afrika uliofanyika pembezoni mwa mkutano wa 29 wa nchi wanachama wa mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi (COP-29) unaofanyika katika Mji wa Baku nchini Azerbaijan.

“Licha ya Tanzania kuwa na hazina kubwa ya rasilimali kijani pamoja na madini ya kimkakati ambayo ni muhimu kwa mabadiliko kuelekea nishati safi, uhifadhi bionuai, uhifadhi wa kaboni, udhibiti wa uchafuzi wa mazingira na uhifadhi wa rutuba ya udongo lakini bado rasilimali hizo hazijajumuishwa katika pato la Taifa, ”amesema.

Ameongeza: “Tanzania inaendelea na uwekezaji ili kuongeza upatikanaji wa nishati mbadala kama vile jotoardhi, nishati ya jua na upepo. Hata jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kukabiliana na nishati chafu ya kupikia ambayo imekua chanzo cha ukataji miti na upotevu wa hifadhi ya kaboni inayopelekea uharibifu wa rasilimali za kijani.”

Dk Mpango amesisitiza ushirikiano wa kikanda katika utunzaji na uendelezaji wa rasilimali kijani barani Afrika, kama vile misitu, madini ya kimkakati na vyanzo vya nishati safi, ni muhimu kwa kuwa rasilimali hizo zina mwingiliano wa karibu unaovuka mipaka ya nchi.

Pia, ametoa wito kwa nchi za Afrika kuwa na sera rafiki zinazoendana zitakazowezesha matumizi endelevu na uwekezaji katika rasilimali za kijani barani humo.

Akizungumzia kauli hizo, mwanaharakati wa mazingira na mwanasayansi ya jamii, Shamim Nyanda amesema hata viongozi wengine wa Afrika wamekuwa wakisisitiza biashara ya kaboni na si tu Tanzania.

Amesema Tanzania inaweza kunufaika na kufaidika kwa kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi ili kuongeza uhifadhi wa kaboni kupitia miradi kama ya upandaji wa miti na miradi mbalimbali ya nishati safi, sambamba na uhifadhi wa bahari na ardhi na utunzaji wa misitu.

“Kuna kaboni ya kijani kama misitu, nishati safi na ardhi na kaboni ya bluu inayohusu bahari, mwani na hata mikoko kwa hiyo inategemea kwa namna gani tunaweza kujiweka kwenye soko la biashara hii kama nchi na bara kwa ujumla kuweza kupeleka bidhaa zetu kuwa bora zaidi kwenye soko la kimataifa.

Nyanda amesema katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,  ni lazima kuangalia namna ya kutunza rasilimali kijani ikiwemo misitu, bahari na vyanzo vya maji.

Amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kuwa na utajiri wa maliasili hivyo inaweza kuimarisha biashara ya kaboni kupitia juhudi za uhifadhi kuendelea kupambana na mabadiliko ya tabianchi ambapo italeta ajira maeneo ya vijijini na kukuza uchumi.

Katika hatua nyingine katika mkutano huo Serikali ya Tanzania imeendelea kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta ya uchumi wa buluu zinazopatikana nchini ikiwemo kupitia mkutano wa pembezoni wenye ajenda inayohusu uvuvi endelevu na uchumi wa buluu.

Lengo la mkutano huo ni kutangaza sekta ya uvuvi na juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Dk Mwinuka Lutengano mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) amesema kama nchi imeweka miongozo mizuri katika sekta ya hiyo, hivyo cha muhimu ni kuunganisha uchumi huo na ule wa kijani ili kuweza kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Amesema nchi lazima ijipange kwa kiasi kikubwa ili itakapoanza miradi ya ubia kutoka nje ya nchi ikiwa ni matokeo ya kuutangaza kama inavyofanywa hivi sasa,  basi iweze kutekelezwa vizuri.

“Tunapaswa kuandaa wataalamu wa kutosha, tuendelee kujiandaa tukae mkao mzuri wa kuwajengea uwezo watu watakaosimamia miongozo ambayo tayari ipo kwa ajili ya wawekezaji watakaokuja kuwekeza sekta ya uchumi wa buluu,” amesema.

Related Posts