Hirizi ya mganga yamponza,  ajisalimisha polisi kukiri mauaji

Arusha. Hirizi ya mganga yamponza, aenda kujisalimisha polisi, kukiri kuua akiamini hatochukuliwa hatua.

Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya Mahakama ya Rufani kubariki adhabu ya kunyongwa hadi kufa dhidi ya Ester Shirima, mkazi wa Moshi,  baada ya kukutwa na hatia ya kumuua Anitha Kimario, kisha kuzika mwili wake kwenye mashamba ya miwa.

Wakati Mahakama hiyo iliyoketi Moshi ikibariki adhabu hiyo kwa Esther, imewaacha huru warufani wenzake wawili, Fredy Mauge na Wilfred Silayo, waliokuwa wamehukumiwa adhabu hiyo ya kifo, baada ya kujiridhisha kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha kesi hiyo dhidi yao.

Katika mahakama ya awali iliyosikiliza na kutoa hukumu hiyo dhidi ya Ester, katika kumtia hatiani mahakama hiyo iliegemea maelezo yake (Esther) ya onyo ambayo alikiri kutenda kosa hilo, licha ya kuja kukana maelezo hayo mahakamani wakati kesi inasikilizwa.

Mbali na maelezo ya Esther, mashahidi wengine wawili wa upande wa mashitaka ambao walidai kumsaidia kukutana na mganga ambaye alimpa hirizi zilizolenga kufukuza nia yoyote ya kumshitaki hata kama angejitokeza na kukiri.

Katika maelezo hayo ya onyo yaliyokuwa yamepokelewa kama kielelezo cha tatu, Esther amenukuliwa akieleza alikuwa alifahamiana na marehemu na walishirikiana katika baadhi ya biashara, ikiwemo biashara haramu alizokuwa akifanya na warufani wenzake za dawa za kulevya.

Amenukuliwa kuwa wakati huo walikuwa wakikabiliwa na kesi ya jinai ya kukutwa na dawa za kulevya, katika Mahakama ya Wilaya ya Bomang’ombe na kwa namna fulani hakukuwa na maelewano mazuri baina yake na marehemu kuhusu masuala ya fedha.

Maelezo hayo yameongeza kuwa Anitha alikasirika kuhusu fedha alizokuwa akimdai Esther, na kumuahidi kuwa ataenda kutoa ushahidi dhidi yao katika kesi iliyokuwa inawakabili, hivyo Ester akawataja Fredy na Wilfred kuwa aliwalipa kwa ajili ya kumuua Esther ambaye mwili wake ulikuja kupatikana Machi 2, 2017.

Baada ya mwili wa marehemu kupatikana, Esther alipigiwa simu na kujulishwa kuwa marafiki wote wa marehemu wanakamatwa, hivyo kumtaarifu Fredy ambaye alimtaka akimbie, ambapo alikimbilia mkoani Tanga.

Maelezo hayo yameeleza kuwa akiwa Tanga kutafuta nguvu za kishirikina, alikutana na Hassan Athuman aliyempeleka kwa mganga ambaye alimweleza hata akijisalimisha polisi, hataweza kushitakiwa kwa kosa hilo, ambapo Ester alifuata maelekezo hayo na kujisalimisha polisi.

Ester, Fredy na Wilfred, walihukumiwa adhabu hiyo na Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi (baada ya kupewa mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ya mauaji), Oktoba 9, 2020 ambapo walidaiwa kumuua Anitha Februari 27, 2017 na kuzika mwili wake katika kitongoji cha Kiyungi Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, Ferdinand Wambali, Ignas Kitusi na Paul Ngwembe walisikiliza rufaa hiyo namba 581 ya mwaka 2020 na kutoa uamuzi huo Novemba 14, 2024, katika vikao vyake vilivyoteki Moshi.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote na kupitia mwenendo wa shauri la awali, rufaa dhidi ya Fredy na Wilfred imekubaliwa, hivyo wameshinda na Mahakama imeamuru waachiliwe huru isipokuwa kama wataendelea kushikiliwa kwa sababu nyingine halali za kisheria.

Jaji Kitusi amesema rufaa dhidi ya mrufani wa kwanza (Esther) imekataliwa (ameshindwa) na kwa upande wake rufaa yake imetupiliwa mbali.

“Kando na maelezo ya onyo iliyobeba maelezo ambayo hakuna mtu ila mrufani (Esther) pekee angeweza kujua, hatuna sababu kutoamini shahidi wa pili, kwani Ester alimwambia shahidi wa pili kwamba alikuwa pale kukiri, hivyo kuna maungamo ya kukiri kwa mdomo mbele ya shahidi wa pili na yale yaliyoandikwa kwa shahidi wa tatu,” amesema Jaji.

Warufani hao watatu walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi (baada ya kuongezewa mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo) wakikabiliwa na kosa la mauaji, kutiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa.

Anitha alidaiwa kutoweka nyumbani kwa siku kadhaa na kusababisha hofu kwa dada yake mkubwa, Evenlight Emanuel (shahidi wa nne) na mtoto wake, Nancy Kimaro ambaye alikuwa akiishi na Evenlight jijini Arusha.

Ilidaiwa na upande wa mashitaka kuwa gari lililokuwa na namba za usajili T 728 CUW aina ya Toyota Rav4 ambalo marehemu alikuwa akilitumia kabla ya kifo chake, halikuwepo.

Ilidaiwa gari hilo la Anitha lilikuwa limetelekezwa eneo la Bomang’ombe na Inspekta Benard alipata taarifa za gari hilo kutelekezwa na kulikuwa na nyaraka zinazolihusisha na Anitha kuwa mmiliki.

Ilidaiwa taarifa hizi zilimwezesha Inspekta huyo kuwasiliana na binti wa marehemu na dada wa marehemu na baadaye Machi 2, 2017 mwili wa marehemu uligunduliwa.

Shahidi wa kwanza, Dk Alex Mremi ambaye ni daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili huo Machi 3, 2017, alieleza kuwa kifo hicho hakikuwa cha asili ingawa hali ambayo mwili huo ulikutwa nayo ilifanya iwe vigumu kufanya uchunguzi kwa uhakika ikiwa kifo kilisababishwa na kunyongwa au kupigwa na kitu kizito kifuani.

Ilidaiwa Machi 6, 2017, Ester (mrufani wa kwanza) aliyekuwa na Hassan Athumani, alijisalimisha kwa shahidi wa pili wa kesi hiyo, Inspekta Msaidizi Sweet Betha kuhusiana na mauaji hayo.

Shahidi huyo alidai Ester alitaka kukutana na Mkuu wa Upelelezi mkoa (RCO), kwa sababu alisikia wanamtafuta na alitaka kujisalimisha kuhusiana na mauaji ya Anitha.

Shahidi huyo alidai kumtia mbaroni na kumpekua kwa mujibu wa taratibu za polisi, ambapo alipata tiketi za basi kutoka Tanga kwenda Moshi moja ikiwa na jina la Ester na nyingine jina la Hassan.

Shahidi huyo alidai kumjulisha RCO kuhusu kilichotokea ambapo aliagizwa kumpeleka mtuhumiwa katika ofisi ya mkuu wa upelelezi wa wilaya ambapo maelezo ya onyo ya Ester yaliandikwa, maelezo yaliyopokelewa kama kielelezo cha tatu ambapo alikiri kutenda kosa hilo.

Aidha, kwa mujibu wa shahidi wa tano na sita, walidai Fredy na Wilfred pia walikiri katika maelezo yao, ambapo licha ya kuyawekea pingamizi wakati wa usikilizwaji wa kesi, yalipokelewa kama kielelezo cha tano na sita, maelezo yaliyokuja kuondolewa kwenye mwenendo wa shauri hilo na Mahakama ya Rufani.

Akijitetea katika kesi hiyo, Esther alikana kuhusika na mauaji ya Anitha na kudai Machi 5, 2017 alirejea nyumbani kutoka kwenye shughuli zake za kila siku, alipewa taarifa na mama yake kuwa polisi walikuwa wakimtafuta na kushangaa kushikiliwa akituhumiwa kumuua rafiki yake.

Esther alidai kuwa Machi 7, 2017 alilazimishwa kusaini maelezo ya kukiri mauaji hayo, lakini alikana kukiri kosa hilo na kukanusha kufahamiansa na Fredy na Wilfred.

 Katika utekelezaji wa mauaji hayo, alidaiwa kuwezesha kumlipa mhusika kutekeleza mauaji hayo.

Aidha,  alidai anamfahamu Fredy ambaye alikutana naye hospitali ya Machame baada ya kuhusika katika ajali ya barabarani iliyohusisha gari lake,  huku kuhusu Wilfred akidai alimfahamu tangu mwaka 2015 katika shughuli zake za biashara.

Aidha Hassan na Juma Mhina walishindwa kupatikana kwa ajili ya kutoa ushahidi wao ambapo maelezo yao yalitolewa kwa ushahidi kama kielelezo cha nane na tisa.

Maelezo hayo yalidaiwa kuunga mkono kesi ya upande wa mashitaka ambayo yalidai kuwa Esther alisafiri hadi Tanga na kukutana na watu wawili waliomsaidia kukutana na mganga,  ambaye alimpa hirizi zilizolenga kufukuza nia yoyote ya kumshitaki hata kama angejitokeza na kukiri.

Fredy, alidai kukamatwa Machi 2, 2017 akiwa Arusha na kuhojiwa kuhusu kifo cha Anitha na kuhamishiwa Moshi Machi 23, 2017  na kukana kutoa maelezo yoyote ya onyo licha ya vitisho na mateso.

Wilfred alidai kukamatwa Machi 18, 2017 wilayani Rombo na kukana kumfahamu Anitha, ambapo alipofikishwa mahabusu Moshi ambapo alikaa kwa siku mbili kabla ya kupelekwa chumba alichokitaja kuwa ni cha mateso alipokutana na warufani wenzake na kudai kulazimishwa kusaini maelezo ya onyo.

Katika kuwatia hatiani, mahakama iliegemea maelezo yake yao ya onyo ambapo Ester alitiwa hatiani kwa kufadhili mauaji ya Anitha huku Fredy akitiwa hatiani kwa kuwa muuaji halisi na Wilfred kwa kumuajiri Fredy kutekeleza mauaji hayo.

Katika rufaa hiyo warufani hao walikuwa na sababu tano za rufaa ikiwemo Mahakama kukosea kisheria kwa kuwatia hatiani kupitia ushahidi wa shahidi wa tano na sita na kielelezo cha nne (gari la marehemu), ambavyo havikusomwa kuwa vitatumika katika kesi hiyo.

Nyingine ni mahakama ilikosea kisheria kuwatia hatiani kulingana na maelezo ya onyo ambayo hayakuwa yamerekodiwa bila utaratibu na kuwa ushahidi wa upande wa mashitaka ukiwa wa kupingana, wa ajabu, hautoshi, haukubaliki hivyo haukuthibitisha kosa hilo bila kuacha shaka.

Warufani hao waliwakilishwa na mawakili watatu wakiongozwa na Charles Mang’anyi huku upande wa mjibu rufaa (Jamhuri) ukiwakilishwa na mawakili watatu wakiongozwa na Wakili Grace Madikenya.

Related Posts