Jengo laporomoka na kuuwa kadhaa Karikakoo Dar es Salaam – DW – 16.11.2024

Mpaka Sasa watu watano wamethibitishwa kupoteza maisha, baada ya jengo la ghorofa nne kuporoka katika eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Hayo yameelezwa Jumamosi na Mrakibu Msaidizi wa Polisi Peter Mtui ambaye anasimamia zoezi la uokoaji katika jengo hilo.

Wakati huo huo Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi amesema wamepokea majeruhi 42 mpaka sasa. 

Soma pia: Jengo laporomoka Kariakoo, Dar es Salaam

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Kassim amefika katika eneo hilo na kuzungumza na wanahabari akisema zoezi la uokoaji linaendelea ili kuhakikisha waliofunikwa na kifusi wanatoka wakiwa hai. 

Dar es Salaam Tanzania | Jengo la ghorofa laporomoka | Waziri Mkuu Majaliwa
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiziungumza na wakaazi alipotembelea eneo la tukio.Picha: Eric Boniphace/DW

“Rais wetu Samia Suluhu Hassan amenituma kuwaambia poleni. Lakini lugha moja tunayoweza kuitoa kwa sasa ni kuwa tunaendelea na uokoaji. Tunaendelea na uokoaji kwa njia nyepesi ili tusilete madhara zaidi kwa walio chini”, amesema. 

Waziri Mkuu amesema serikali kwa sasa imehamia katika eneo hilo kwa ajili ya kuhakikisha zoezi la uokoaji linafanyika.

Amesema takriban viongozi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu , ambao ndio walio katika kamati ya ulinzi, usalama na majanga, wapo katika eneo hilo kuhakikisha zoezi linafanyika kwa umakini.

Soma pia: Serikali ya Tanzania yaunda tume na wafanyabiashara

“Nikiwa hapa nimeona wapo watu wanaendelea kutolewa wakiwa hai, walioko chini wanawasiliana na ndugu zao na sisi tunajua wapi pa kueleketa uokoaji. Neno kubwa ni pole kwa watanzania na jamii ya wafanyabiashara  Kariakoo,”amesema. 

Dar es Salaam Tanzania| Mporomoko wa jengo Karikakoo.
Wafanyakazi wa uokozi wakimbiza mmoja ya waliotolewa kwenye kifusi kwa ajili ya kumpatia huduma ya kwanza.Picha: Eric Boniphace/DW

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara na Seleman Jaffo aliyekuwa eneo la tukio amesema jitihada za uokoaji zinaendelea. 

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amezungumza na DW na kuwataka wafanyabiashara na watanzania kuwa watulivu kwani serikali inafanya kila mbinu ili kuwaokoa walio chini ya jengo. 

Related Posts