Kapilima akomalia mastaa KenGold | Mwanaspoti

KOCHA wa KenGold, Omary Kapilima amesema kipindi hiki ambacho Ligi Kuu Bara imesimama, anaendelea na jukumu kubwa la kuhakikisha anatengeneza balansi nzuri ya kikosi hicho, kuanzia eneo la uzuiaji na ushambuliaji ambalo lina changamoto.

Kapilima amezungumza hayo wakati kikosi hicho kikiburuza mkia katika msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi tano baada ya kushinda mchezo mmoja kati ya 11 iliyocheza. Imepoteza michezo minane na sare mbili.

Kwa sasa KenGold inajiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal Union utakaochezwa Novemba 23 mwaka huu kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

“Tunapambana kuendelea kupata michezo angalau miwili hadi mitatu ya kirafiki ili kujiweka fiti zaidi, msimu huu kwetu umekuwa ni mgumu na ukiangalia ushindani pia umeongezeka kwa kila timu, hivyo ni lazima tuanze kuamka mapema,” alisema.

Kapilima aliongeza, licha ya muda mchache aliokuwa nao ila atahakikisha anapambana kutengeneza eneo lote la ushambuliaji kwani katika michezo mitatu aliyoiongoza timu hiyo, ameona kuna mwelekeo mzuri unaoweza kumpatia matokeo chanya mbeleni.

Kocha huyo aliyefundisha na kucheza timu mbalimbali hapa nchini zikiwemo Majimaji, Yanga na Mtibwa Sugar, amejiunga na kikosi hicho Oktoba 22 mwaka huu akichukua nafasi ya Fikiri Elias aliyeamua kuondoka mwenyewe Septemba 17, mwaka huu.

Fikiri aliondoka kutokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo ambapo aliiongoza katika michezo mitatu tu ya Ligi Kuu Bara na kati yake alipoteza yote akianza kufungwa 3-1 dhidi ya Singida Black Stars, Fountain Gate (2-1) kisha KMC (1-0).

Baada ya hapo kikosi hicho kikaongozwa na Jumanne Challe aliyeipandisha timu hiyo Ligi Kuu Bara kutokea Ligi ya Championship na katika michezo yake mitano aliyoiongoza alishinda mmoja akitoa sare mmoja na kupoteza mitatu.

Kitendo cha Challe kutokuwa na sifa za kusimamia benchi la ufundi kwa zaidi ya michezo mitano ya Ligi Kuu Bara, ndipo Kapilima akajiunga na timu hiyo na kukiongoza katika mechi tatu akianza na kichapo cha mabao 4-1 dhidi ya Azam FC. Baada ya hapo, timu hiyo ikatoka sare ya mabao 2-2 na Dodoma Jiji, kisha mechi ya mwisho ikachapwa bao 1-0 na Tanzania Prisons.

Related Posts