Kilosa. Mtoto mchanga mwenye umri wa siku moja amekutwa amefukiwa kwenye shimo huku kichwa kikiwa nje katika eneo la Manzese, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro huku wananchi wakihoji sababu za mama wa mtoto huyo kufanya ukatili huo.
Mashuhuda wa tukio hilo wamesema taarifa za mtoto huyo ziliibuliwa na wapita njia, saa 4 asubuhi, baada ya kusikia kilio chake kutoka kwenye kichaka kilicho karibu na makazi ya watu.
Mmoja wa mashuhuda hao, Everina Dominiki, ameeleza namna alivyosikia kilio cha mtoto huyo na hatua alizochukua.
“Nilikuta sehemu ya uso tu ndiyo ilikuwa wazi, lakini mwili mzima ulikuwa umefukiwa, nilipomwona, nilimwita bosi wangu na watu wengine waliokuwa wakipita ili kumsaidia,” amesema Everina.
Ameongeza kuwa ni muhimu kuzuia mimba zisizotarajiwa kwa kutumia kinga ili kuepusha matukio kama hayo kwa wanawake wanaojifungua.
“Wasichana wenzangu, ni muhimu kuchukua hatua mapema ili kuepuka matukio kama haya. Huu ni ukatili mkubwa,” amesema Everina.
Zuberi Hassan, kijana aliyehusika kumfukua mtoto huyo amesema waliendelea kumfukua mtoto huyo kwa tahadhari na kisha kumkimbiza hospitali ya wilaya kwa matibabu.
“Tulimkuta akiwa amefungwa na kipande cha kanga, kilichotushtua zaidi ni kwamba mtoto alikuwa na kondo lake, jambo linaloashiria kuwa mama alijifungua salama ila baadaye aliamua kumfukia kwa makusudi shimoni, tulihakikisha anakimbizwa hospitalini mara moja,” amesema Zuberi.
Zuberi ametumia fursa hiyo kutoa ujumbe wa kuhamasisha uwajibikaji wa wazazi wanaopata watoto wasiotarajiwa.
“Kama umeweza kutunza mimba kwa miezi tisa, tafadhali jitahidi kumtunza mtoto, kuwa na mtoto ni baraka, na kumtupa ni dhambi kubwa mbele za Mungu,” amesema.
Ofisa Tarafa wa Wilaya ya Kilosa, Prepetua Mgasi amethibitisha kupokea taarifa za tukio hilo na kusema kuwa hatua stahiki zitachukuliwa. Amesema endapo mama wa mtoto huyo hatajitokeza, Serikali itampeleka mtoto kwenye kituo cha kulelea watoto.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kilosa, Dk Gibui Lambo ameeleza mtoto huyo yuko katika hali nzuri baada ya kupatiwa huduma ya kwanza.
“Kwa sasa mtoto anapata matibabu na hali yake inaendelea kuimarika,” amesema Dk Lambo.