Lema adai vurugu za Arusha zilipangwa, aagiza wahusika kuvuliwa uanachama

Arusha. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amedai vurugu zilizojitokeza juzi wakati wa uchaguzi wa viongozi wa Mkoa wa Arusha, zilipangwa kwa lengo la kuharibu uchaguzi huo.

Ameagiza viongozi wa mikoa na wilaya wanakotoka waliosababisha vurugu hizo, kuwasiliana na matawi wanayotoka na kuwavua uanachama kwa madai kuwa wamekidhalilisha chama hicho.

Lema ameyasema hayo leo Juammosi Novemba 16, 2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni siku chache tangu itokee sintofahamu, baada baadhi ya wanachama wa chama hicho kuleta vurugu wakituhumu uchaguzi huo kugubikwa na rushwa.

“Ninaagiza viongozi wa chama, kwa yeyote aliyehusika kwa sababu wapo waliotoka Mkoa wa Kilimanjaro, walikuja kufanya fujo na kusababisha taharuki kubwa na udhalilishaji kwa chama chetu, wachukuliwe hatua za kuvuliwa uanachama katika matawi yao mara moja  kwa sababu wamekidhalilisha chama,” amesema.

Lema amesema alipanga kutozungumza juu ya suala hilo ila amelazimika kufanya hivyo,  baada ya kuona anachafuliwa jina lake pamoja na suala hilo kuleta taharuki kwa wanachama.

Amedai kuwa fujo zilizotokea kwenye uchaguzi huo zilipangwa kwa lengo la kuharibu uchaguzi na kudai kuwa kabla ya vurugu hizo, polisi walifika eneo hilo na kudai wamepata taarifa kuwa kuna fujo, ambazo baadaye vurugu zilipoanza polisi pia walifika eneo hilo.

“Ukitaka kufahamu lile suala lilipangwa, wakati lile tukio linaanza waliokuja kufanya masuala yale walikuja wameambatana na waandishi wa habari, nina uhakika lile jambo lilipangwa na lilipangwa kuharibu uchaguzi wa Arusha.

“Walipokuja kule ukumbini na kuanza kupiga kelele niliambiwa walitolewa kule juu ukumbini wakasema wanataka kukaa kwenye swichi ya umeme na wakawa wanaongea maneno ya kejeli sana,” amedai.

 “Lengo lilikuwa ni kuharibu mkutano na walioshinda wasishinde, na hii ilikuwa imepangwa…ndiyo maana waandishi na nyie mlipatikana, kwa muda unaofaa na mlikuwa mmejiandaa, mkaja na tochi, mlijua ni tukio la usiku,” amesema.

Uchaguzi huo uliokuwa ukisimamiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Benson Kigaila, ambapo Lema amedai alilazimika kumuomba Kigaila ateremke akawazuie waliokuwa wanafanya fujo kwani mmoja wao ni rafiki yake mkubwa.

Lema amedai siku chache zilizopita, mwanachama mmoja  akiwa na wenzake walifanya fujo kwenye uchaguzi wa Monduli mpaka uchaguzi ukaahirishwa.

“Msimamizi wa Monduli alinipigia nikampa simu akaongea na Kigaila, akidai wanataka kumpiga, wamepora na matokeo ya mabaraza, kesho yake nikiwa na Kigaila, (anataja jina)  akampigia simu (Kigaila), akaongea naye kama dakika 20, nikamwambia Kigaila hawa watu wamefanya fujo, wamedhalilisha watu, unapowapa nafasi, unatunyima mamlaka ya kichama ya kuwachukulia hatua,” amedai Lema.

Lema ameeleza kushangazwa na yeye kunyooshewa kidole badala ya kamati nzima,  na kuwa walikuwa wanalenga kuchafua jina lake na kuwa hajawahi kwenda jimbo au kata yoyote kuratibu masuala ya upatikanaji wa viongozi na kuwa hajapanga kiongozi yeyote katika mchakato huo.

“Mnaweza kusema kwanini haya mambo msiongee kwenye vikao vya ndani, haya yataongelewa kwenye vikao vya ndani na lazima yaongelewe nje kwa sababu yameshaharibu taswira za watu, nimetukanwa na kudhalilishwa sana na haya maneno yako barabarani,” amedai.

Kuhusu tuhuma za kuwa chanzo cha vurugu za uchaguzi huo, Lema amekana tuhuma hizo akieleza kuwa alishatangaza kuwa hana mpango wa kugombea nafasi yoyote kwenye uchaguzi ngazi ya kanda katika chama hicho, hivyo hana sababu ya kupanga timu kuelekea uchaguzi ndani ya chama hicho.

“Kama nilivyosema, sigombei nafasi yoyote kwenye kanda, nasisitiza sigombei nafasi yoyote ndani ya chama katika kanda hii,’’amesema.

Related Posts