Ligi Kuu Tanzania Bara imeheshimishwa na nyota wa kigeni wanaochezea timu tofauti za taifa, baada ya vikosi vyao vingi kufanikiwa kutinga fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazofanyika Morocco mwakani.
Mechi za raundi ya tano ambazo zimechezwa kuanzia Jumatano wiki hii, zimeonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa ongezeko kwenye Afcon 2025 la timu za taifa ambazo baadhi ya nyota wao wanacheza Ligi Kuu Tanzania Bara.
Timu za taifa ambazo zimefuzu Afcon 2025 huku vikosi vyao vikiwa na wachezaji wanaocheza Ligi Kuu Bara ni Uganda, Zimbabwe, Burkina Faso, Mali na Zambia.
Burkina Faso ambayo wanachezea nyota wa Yanga, Stephane Aziz Ki na mwenzake wa Simba, Valentine Nouma ilijihakikishia tiketi ya Afcon 2025 kabla hata ya raundi ya tano ikipenya kupitia kundi L sambamba na Senegal.
Hata hivyo katika mchezo wa raundi ya tano juzi Alhamisi dhidi ya Senegal, BurkinaFaso ilipoteza kwa bao 1-0.
Ushindi wa bao 1-0 ambao Zambia iliupata nyumbani, jana Ijumaa, Novemba 15 dhidi ya Ivory Coast uliihakikishia tiketi ya kucheza Afcon mwakani.
Kennedy Musonda ndio alifunga bao hilo pekee la Zambia ambayo pia anacheza pamoja na nyota mwenzake wa Yanga, Clatous Chama na staa wa Simba, Joshua Mutale.
Zimbabwe ya Prince Dube nayo imefuzu Afcon baada ya jana kulazimishwa sare ya bao 1-1 nyumbani na Kenya ambayo imeifanya ifikishe pointi tisa na hivyo kuwa na uhakika wa kumaliza katika nafasi mbili za juu kwenye kundi J pamoja na Cameroon.
Uganda licha ya kufungwa mabao 2-0 nyumbani na Afrika Kusini jana, ilifuzu kufuatia ushindi wa mabao 3-2 ambao Sudan Kusini iliupata mbele ya Congo juzi.
Uganda ambayo anachezea Steven Mukwala wa Simba na Khalid Aucho wa Yanga, imefuzu kupitia kundi K pamoja na Afrika Kusini.
Timu nyingine iliyofuzu ambayo ina mchezaji anayecheza Ligi Kuu Bara ni Mali anayochezea kipa wa Yanga, Djigui Diarra.
Ushindi wa bao 1-0 ambao Mali iliupata ugenini dhidi ya Msumbiji, umeifanya ifikishe pointi 11 zilizoihakikishia tiketi ya Afcon 2025 kupitia kundi I.
Timu 19 ambazo zimeshafuzu Afcon ni Morocco, Algeria, Misri, Tunisia, Mali, Angola, Nigeria, Afrika Kusini, Uganda, Burkina Faso, Senegal, DR Congo, Cameroon, Zimbabwe, Zambia, Ivory Coast, Comoro, Guinea ya Ikweta na Gabon.