NEEC yawaita wadau uwezeshaji wananchi kiuchumi

Dar es Salaam. Wadau takribani 700 wa  masuala ya uwezeshaji wananchi kiuchumi wanatarajiwa kukutana jijini Dodoma,  kwa siku mbili kufanya tathmini ya utekelezaji wa mikakati ya uwezeshwaji wa wananchi pamoja na changamoto zake.

Hayo yamebainishwa leo Novemba 16, 2024 na Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng’i Issa katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Beng’i amesema wadau hao watakutana kupitia kongamano la nane la uwezeshwaji wananchi kiuchumi linalotarajiwa kufanyika Disemba Desemba 3-4 mwaka huu.

Amesema kongamano hilo litahusisha wizara, mashirika, wakala na taasisi za Serikali, taasisi binafsi chini ya mwamvuli wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), mikoa, halmashauri, wajasiriamali, taasisi za fedha, taasisi za elimu, watafiti, wawekezaji pamoja na wadau wengine wa masuala ya uwezeshaji.

Ameeleza kuwa kupitia midahalo mbalimbali itakayofanyika katika kongamano hilo,  watajadili namna ambavyo wananchi wanaweza kunufaika na fursa mbalimbali zinazojitokeza kujikwamua kiuchumi.

Pia ameeleza kuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa  anatarajiwa kuwa mgeni rasmi wa kongamano hilo  linaloongozwa na kauli mbiu isemayo: Uwezeshaji wananchi kiuchumi ni msingi wa maendeleo ya Tanzania

“Kongamano litatoa pia fursa ya kutathmini utekelezaji wa sera ya uwezeshaji pamoja na taarifa mbalimbali ya utekelezaji wa mambo yaliyokuwa kwenye kongamano la saba,”amesema.

Ameongeza kuwa wakati wa kongamano, tuzo pia zitatolewa kwa wote waliofanya vizuri ikiwemo mkoa uliofanya vizuri, wajasiriamali na taasisi  mbalimbali za uwezeshaji,   kwani mafanikio mengi yameshapatikana chini ya Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi.

Related Posts