Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameleza kusikitishwa na taarifa ya ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa katika Kata ya Kariakoo, Wilaya ya Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam akiagiza kuongezwa kwa nguvu ya uokoaji.
Ajali ya kuanguka ghorofa imetokea leo Novemba 16, 2024 saa tatu asubuhi iliyosababisha vifo na majeraha kwa wafanyabiashara wa jengo hilo hata hivyo mpaka sasa idadi rasmi bado haijatolewa.
“Nimeuagiza uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, na Idara ya Menejimenti ya Maafa kufanya kila linalowezekana kufanikisha zoezi la uokoaji na tiba kwa majeruhi,” amesema Rais Samia katika salamu zake za pole.
Katika salamu hizo pole alizozituma kupitia mtandao wa kijamii, Rais Samia amehimiza Watanzania kuendelea kuwaombea wale wote ambao wamekumbwa na ajali hiyo.
“Wakati hilo likiendelea na tukimuomba Mwenyezi Mungu awape pona ya haraka majeruhi, tuwaombee pia utulivu na subira ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wenzetu wanaotafuta riziki zao katika eneo hili muhimu kibiashara nchini ambao kwa namna mbalimbali wameathiriwa na ajali hii”
Aidha mpaka sasa uokoaji unaendelea katika eneo hilo, magari ya wagonjwa kutoka sehemu mbalimbali kwa ajili ya kubeba majeruhi ndiyo yaliyotawala eneo hilo.