YANGA imemtambulisha rasmi kocha Mjerumani Sead Ramovic kama mbadala wa Miguel Gamondi waliyeachana naye rasmi jana, Ijumaa mchana.
Sead anajiunga na Yanga baada ya kuachana na TS Galaxy ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini wiki moja iliyopita.
Alijiuzulu baada ya sare ya 1-1 dhidi ya Stellenbosch ikiwa ni mechi sita mfululizo bila ushindi katika ligi msimu huu.
Sare hiyo ya jijini Cape Town ikiwa ni alama yao ya pili pekee katika kampeni zao. Mechi ijayo ni dhidi ya Sekhukhune United Novemba 26, baada ya mapumziko ya kimataifa ya Fifa.
Akizungumza kwenye mahojiano maalumu na Gazeti la iDiski Times la Afrika Kusini, Ramovic aliweka wazi kwamba anataka makombe na haoni uelekeo wa kuyapata Galaxy kutokana na mambo yanavyokwenda.
“Nazingatia njia inayolingana na malengo na matarajio yangu kama kocha, klabu hii inaendesha shughuli zake kwa kutegemea mauzo ya wachezaji kujikimu. Imenipa mengi, lakini tamaa yangu ya kushindania mataji kwenye viwango vya juu zaidi inahitaji mwelekeo tofauti mahali ambapo kuna utulivu wa kifedha wa kuweza kufanikisha hilo,” alisema Ramovic katika mahojiano hayo.
“Nataka kuongoza timu yenye uwezo na rasilimali za kushindana kuwania mataji jambo linalohitaji utulivu wa kifedha na uwekezaji wa muda mrefu.
“Nina njaa ya mafanikio, ari na kujituma kupindukia kushindana katika kiwango cha juu zaidi na nimejidhatiti kuona wapi shauku yangu inaweza kunifikisha. Uamuzi huu haujatokana na kutoridhika, bali ni hamasa ya kujipima na kufikia upeo wangu wa juu zaidi.
“Mahusiano yangu na mwenyekiti pamoja na kila mmoja katika klabu hii yamebaki kuwa ya heshima kubwa. Hapa nimejifunza kukabiliana na changamoto zilizoboresha ujuzi na uthabiti wangu.
“Kushinda mataji si lengo la mwisho tu, bali ni uthibitisho wa kazi ngumu, kujitolea, na dhamira isiyoyumba,”anasisitiza Kocha huyo.
Kocha huyo ana umri wa miaka 45. Alicheza klabu mbalimbali za ligi za Ujerumani, Norway, Denmark, Serbia na Ukraini kama kipa kabla ya kuhamia kwenye ukocha mwaka 2021-24 akiwa na TS Galaxy ya Afrika Kusini.
Aliiongoza timu hiyo kwa miaka mitatu akionyesha umahiri wa kufundisha na kukuza vipaji vya vijana.
Kuna kitu Gamondi akifahamu atajuta, iko hivi mabosi wa Yanga wamefichua kwamba timu hiyo ilipokutana na Galaxy Julai 24, 2024 kwenye mchezo wa kirafiki, kocha huyo Muargentina alikubali ufundi wa Mjerumani huyo.
Mchezo huo ambao ulimalizika kwa Yanga kushinda kwa bao 1-0 lakini kumbe mabosi wa timu hiyo wakabeba maneno hayo ya kocha wao ambapo sasa baada ya kusikia ameachana na Galaxy wakamvuta haraka.
Awali, Yanga ilikuwa imchukue kocha Mualgeria Kheireddine Madoui anayeifundisha Costantine ya nchini humo ambaye mabosi wa Jangwani waligoma kuendelea kumsubiri mpaka akamilishe taratibu ndefu za kuvunja mkataba wake wa sasa.
Madoui alikuwa anawataka Yanga kusubiri amalizane vizuri na klabu yake ambapo Yanga ikamtaka atulie kwani haitaweza kusubiri zaidi ikihofia kuchelewa maandalizi ya mechi za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika haswa mechi dhidi ya Al Hilal ya Florent Ibenge.