Serikali yaikaribisha sekta binafsi katika ulinzi wa taarifa

Arusha. Serikali imekaribisha sekta binafsi na mashirika ya kimataifa,  kushiriana katika ulinzi wa taarifa ili kukabiliana na ukiukwaji wa faragha unaoathiri sekta mbalimbali nchini.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi kwenye kongamano la wanataaluma wa sheria nchini inayoendelea mkoani Arusha yenye kaulimbiu “Kuimarisha ulinzi wa taarifa katika uchumi na sekta mbalimbali: kujenga njia ya faragha na usalama”.

Mhandisi Mahundi amesema ushirikiano wa pamoja wa Serikali, viongozi mbalimbali, sekta binafsi, wadhibiti na watetezi wa faragha na uhuru wa raia,  utasaidia kubuni mfumo mmoja imara utakaoeshimu faragha za watumiaji wa mitandao dhidi ya hatari kwa hatma ya uchumi wa kidigiti na uhalifu wa mitandaoni.

“Mfumo utakaoheshimu faragha utasaidia watumiaji kuwa huru kwa shughuli zao mbalimbali hasa za uvumbuzi, ubunifu na biashara mbalimbali kwa ajili ya kusaidia uchumi wa kidigitali,” amesema Mahundi na kuongeza:

“Lakini ukosefu wa usalama wa taarifa umekuwa na madhara makubwa katika sekta mbalimbali za umma na binafsi ikiwemo ukiukwaji wa faragha, wizi wa mali na fedha, lakini wengine kutumikishwa na zaidi kuingizwa kwenye matatizo yasiyotarajiwa.’’

Ametumia nafasi hiyo kuwataka wanataaluma wa sheria nchini kusaidia Serikali kusimamia ulinzi wa taarifa,  ili kupunguza hatari wanazokabiliana nazo wananchi hasa uhalifu wa mitandaoni.

Awali, akimkaribisha Waziri, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, (TLS), Boniface Mwabukusi amesema wameitisha kongamano hilo na kuwaalika wataalamu wa masuala ya ulinzi wa taarifa binafsi,  ili kuwanoa wanachama wao juu ya mifumo ya kidigitali na makosa wanayoweza kukumbana nayo dhidi ya taarifa za wateja.

Amesema ulinzi wa taarifa ni eneo linaloitaji nguvu kubwa na maadili ya hali ya juu kwa ajili ya kuboresha haki za faragha za wateja wao, lakini changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni matumizi ya karatasi katika shughuli zao ikiwemo kukusanya ushahidi na utunzaji wa  mwenendo wa kesi.

“Bado usalama ni mdogo sana kwenye shughuli zetu hasa katika matumizi ya teknolojia hivyo kunahitajika sheria madhubuti, kanuni na sera imara ya kujibu changamoto ya tunalindaje au tunahifadhije zile taarifa tulizonazo kwa umakini.

“Mifumo hii inaandaliwa kidunia na sisi tunakuja kutumia lakini tuhakikishe matumizi yetu tunazingatia upatikanaji wa fursa na kuzichangamkia lakini zaidi tutumie katika kujibu changamoto zetu hasa katika sekta mbalimbali za kiuchumi, kibiashara na uhakika wa chakula pia,” amesema.

Akitoa mada katika kongamano hilo, Mkuu wa Kitengo cha Mifumo ya Ulinzi kutoka Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Daniel Sarungi amesema lengo lao ni wataalamu hao kufanya kazi kuendana na mabadiliko ya teknolojia kuanzia jinsi wanavyopeana taarifa, wanavyokusanya ushahidi hadi kuziwasilisha.

Amesema mabadiliko ya teknolojia yamekuja na ulazima wa ujenzi wa ‘mfumo wa ridhaa’ ambao unampa mwananchi haki ya kuona taarifa zake zimetumikaje na wapi na wakati gani, hivyo semina hiyo inawapa mawakili elimu ya kuepukana na makosa hayo.

“Kutokana na mabadiliko haya, kuna sheria ya misingi ya taarifa binafsi ambayo inampa mwananchi fursa ya kuona taarifa zake zimetumikaje na zimetumika wapi na wakati gani, na kama hajui ana haki ya kuwasilisha malalamiko yake tume ya taarifa binafsi na hatua zikachukuliwa dhidi ya mhusika,” amesema.

Related Posts