Dar es Salaam. Watu watano wamefariki dunia na wengine 42 wamejeruhiwa baada ya jengo la ghorofa nne kuporomoka katika makutano ya Mtaa wa Congo na Mchikichi, Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Takwimu hizo ni kwa mujibu wa Mrakibu wa Jeshi la Zimamoto na Ukoaji, Peter Mtui anayesimamia shughuli za uokoaji katika tukio hilo.
Kazi ya uokoaji inatekelezwa na jeshi hilo kwa kushirikiana na vikosi vingine vya ulizi na usalama, likiwamo Jeshi la Polisi na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Ingawa chanzo cha kuporomoka kwa ghorofa hilo bado kinachunguzwa, taarifa kutoka kwa baadhi ya mafundi zinaeleza walikuwa wakichimba ndani ya jengo lililoporomoka kuwezesha eneo la chini kukutana na lingine la jengo jirani.
Kwa mujibu wa mmoja wa mafundi hao, walianza kazi ya kuchimba Novemba 14, 2024 na kwamba, kwa kutumia nyundo walikuwa wanagonga mawe ya kuta.
Hata hivyo, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Ilala, Crispin Ladiuzima aliyekuwa eneo la tukio akizungumza na wanahabari, amesema kwa tathimini ya haraka wameona jengo hilo limelewa na mzigo mkubwa.
“Kumekuwa na maeneo ya mizigo mengi kiasi kwamba uwezo wa jengo umeshindwa kuhimili na kuporomoka, tumesema hivyo kitaaluma unaliona lile jengo lilielemewa,” amesema na kuongeza:
“Kungekuwa ni tetemeko la ardhi na vitu vingine, mara nyingi ghorofa zote tano zingelaliana. Licha ya yote, kazi ya uokozi inaendelea vizuri leo hakuna kuzima moto, tuna imani tutafikia mwisho mzuri.”
Ameshauri majengo yatumike kwa malengo yaliyokusudiwa na endapo yatabadilishwa taratibu, sheria na kanuni zifuatwe kuepuka taharuki na matatizo kama hayo.
Pia ametoa wito kwa wamiliki wa majengo, wakandarasi na mamlaka zinazopitisha ujenzi wa majengo husika kuwe na utaratibu wa ukaguzi wa sehemu husika.
“Mtu anakuja kwako anasema nataka kujenga nyumba ya biashara au makazi, basi na ikatumike hivyo, huku watu wanatabia ya kubadilisha matumizi ya jengo ndiyo athari zake hizo kama hili jengo lilivyojaa mizigo,” amesema.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyefika eneo la tukio na baadaye kuwatembelea majeruhi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), amesema uchunguzi utafanyika kubaini sababu ya jengo hilo kuporomoka.
“Nimewasili pale nimeona ujenzi mpya unaendelea, nimewataka waimarishe yasitokee haya, lile jengo lilikuwa la zamani si jipya, kwa nini limebomoka leo? wataalamu wetu watatuambia,” amesema.
Amevitaka vyombo vya ulinzi kutumia taaluma zao vizuri kuokoa maisha ya wananchi.
Mapema, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Mohamed Janabi amesema majeruhi wote 40 waliofikishwa Muhimbili wamefanyiwa kipimo cha Ultrasound kubaini kama kuna dalili zozote za damu kuvuja ndani ya mwili.
Amesema hospitali hiyo tangu asubuhi imepokea majeruhi 40 na kwamba, 33 wameruhusiwa kurejea nyumbani na saba ndiyo wanaendelea na matibabu.
Akiwa eneo la tukio, Majaliwa amesema majeruhi wengine wamepelekwa katika hospitali za rufaa za mikoa za Temeke, Mwananyamala na Amana.
Salamu, maelekezo ya Samia
Kupitia akauti zake za mitandao ya kijamii, Rais Samia Suluhu Hassan ameandika: “Nimesikitika kupokea taarifa ya ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa katika Kata ya Kariakoo, Wilaya ya Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam.
“Nimeuagiza uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, na Idara ya Menejimenti ya Maafa kufanya kila linalowezekana kufanikisha zoezi la uokoaji na tiba kwa majeruhi.”
Ameandika: “Wakati hilo likiendelea na tukimuomba Mwenyezi Mungu awape pona ya haraka majeruhi, tuwaombee pia utulivu na subra ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wenzetu wanaotafuta riziki zao katika eneo hili muhimu kibiashara nchini, ambao kwa namna mbalimbali wameathiriwa na ajali hii.”
Kwa mujibu wa mashuhuda, ghorofa hilo lilianguka ghafla saa tatu asubuhi wakati mafundi wakiwa kazini kuongeza sehemu ya maduka kwa chini.
“Tulianza kusikia kelele za mtingishiko, kisha kwa ghafla jengo zima likaanguka, wananchi wameshindwa kujiokoa. Kazi ya ujenzi ilianza tangu jana (Novemba 15), hivyo angetaka urahisi angebomoa tu jengo lote,” amesema shuhuda wa tukio hilo, Harrison Shayo.
Ibrahimu Mussa, mmoja wa waokoaji aliyejitambulisha kuwa ni askari wa jiji amesema amewasaidia watu zaidi ya 10 waliokuwa jirani, huku wengine ikielezwa walikuwa bado ndani kwenye korido.
“Nilifika kwenye usawa wa ngazi na kuwasaidia baadhi yao kwa kuwashika mkono na kuwavuta nje. Wengi wao wapo chini na nimetoka kwa sababu ya kuzidiwa na hali ya hewa,” amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Challamila, Profesa Janabi na Naibu Spika, Mussa Zungu ambaye ni mbunge wa Ilala walifika eneo la tukio.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema idadi ya watu waliokolewa ni kubwa na wachache wamepata majeraha.
“Watu wengi wameokolewa na kazi kubwa inaendelea,” amesema.
Katika eneo la tukio, umati ulijitokeza kufanya kazi ya uokozi, huku Jeshi la Polisi likitahadharisha watu kukaa mbali ili kuliachia nafasi lifanye kazi.
Hata hivyo, wananchi waliendelea kusogea katika eneo hilo wengine wakilinda mali zilizotapakaa ardhini.
Pale mtu alipookolewa katika jengo hilo baadhi ya watu waliangua vilio, huku shughuli za biashara katika maeneo ya jirani zikisimama kwa muda.
Kelele za ving’ora vya magari ya wagonjwa ndizo zilizotawala mitaa ya Kariakoo. Kazi ya uokozi inaendelea.