Wabunge wataka wamiliki hoteli kuwatumia wataalamu wazawa wa kahawa

Moshi. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeitaka Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) kuhakikisha hoteli zenye nyota mbili hadi tano zinatumia waandaaji wa kahawa wazawa wenye ujuzi badala ya kutumia wale wa nje.

Imesema kufanya hivyo kutalinda taaluma ya kahawa inayozalishwa hapa nchini na kuleta tija katika sekta hiyo ya kahawa.

Akizungumza leo kwa niaba ya kamati hiyo wakati walipotembelea ofisi za makao makuu ya bodi hiyo zilipo Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro,  Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mariam Ditopile amesema ni muhimu kulinda taaluma hiyo na kuhakikisha vijana wazawa wenye ujuzi huo, wanaleta tija katika mapinduzi ya kahawa nchini.

“Ili kulinda taaluma mnazozalisha lazima mkae na hao wanaotoa vibali vya ajira na kuweka masharti kwamba mmiliki wa hoteli kuanzia nyota mbili hadi tano, barista (mwandaa kahawa) ni lazima awe Mtanzania.”

“Kama yeye anaona hana ujuzi wa kutosha, huyu wa nje aje kumuongezea tu ujuzi, lakini kama nyie mnawafundisha na mnawazalisha wenye uwezo mwishowe wakikosa kazi itakuwa ni tatizo baadaye,” amesema.

Amesema tangu Rais Samia Suluhu Hassan ameingia madarakani, amekuwa ni mwanamapinduzi wa uchumi kupitia sekta ya kilimo, hivyo akaitaka TCB kuendelea kuwa vinara wa huduma ya kahawa Afrika na duniani kote.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TCB, Primus Kimaryo amesema katika kuhakikisha sekta ya kahawa inafanya vizuri, wamejiwekea mikakati mbalimbali wakisimamia maeneo matatu ambayo ni kuongeza tija na uzalishaji, kuongeza kipato cha mkulima na kuweka mazingira mazuri ya biashara.

Amesema kupitia mikakati hiyo, uzalishaji wa kahawa umeongezeka kutoka wastani wa tani 50,000 hadi kufikia tani 70,000, hali ambayo imetokana na sababu mbalimbali ikiwemo Serikali kupitia bodi kusambaza miche ya kahawa bure kwa wakulima pamoja na kutolewa kwa mbolea ya ruzuku.

Related Posts