Wapinzani ni asilimia 38 ya wagombea, CCM yatawala serikali za mitaa

Dodoma. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimefanikiwa kuweka wagombea katika nafasi zote za vijiji, vitongoji na mitaa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa,  huku upinzani ukiweka nafasi 30,977 sawa na asilimia 38 ya nafasi zote 80,430 zinazoshindaniwa.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa leo Jumamosi, Novemba 16, 2024 wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa habari jijini Dodoma, alipokuwa  akitoa tathimini ya uchaguzi wa serikali za mitaa.

Mkutano huo umehudhuliwa pia na wakuu wa mikoa, Adam Malima (Morogoro), Martin Shigela (Geita), Juma Homera (Mbeya), Zainab Telack (Lindi) na Rosemary Senyamule wa Dodoma.

Amesema kwa kuzingatia maeneo ya utawala yaliyotangazwa katika gazeti la Serikali,  Tangazo Na.796 na 797 yote ya Septemba 6, 2024, vijiji vilivyopo ni 12,333, mitaa 4,269 na vitongoji 64,274.

Amesema hata hivyo, kutokana na Halmashauri za Wilaya za Kaliua, Nsimbo na Tanganyika kuwa na makazi ya wakimbizi ya Ulyankulu, Katumba na Mishamo, na wananchi kuhama kwenye baadhi ya vitongoji  kutokana na sababu mbalimbali, maeneo yatakayofanya uchaguzi tarehe 27 Novemba, 2024 kwa sasa  ni  vijiji 12,280, mitaa 4,264 na vitongoji 63,886.

“Hivyo, nafasi zitakazogombewa ni  mwenyekiti wa kijiji nafasi 12,280, mwenyekiti wa mtaa nafasi 4,264 na mwenyekiti wa kitongoji nafasi 63,886, wajumbe wa Serikali ya kijiji 230,834 na wajumbe wa kamati ya mtaa 21,320,” amesema.

Amesema kwa ujumla mwitikio wa vyama vya siasa katika shughuli ya  kuchukua na kurejesha fomu za kugombea, ulikuwa mzuri ambapo vyama vyote 19 vyenye usajili kamili vilijitokeza.

Aidha, katika hatua hiyo amesema Chama cha Mapinduzi kilifanikiwa kuweka wagombea katika nafasi zote zilizogombewa na vyama vingine viliweka wagombea katika nafasi mbalimbali.

Nafasi za mwenyekiti wa kijiji zinazogombewa ni 12,280 ambapo vyama 18 vya siasa viliweka wagombea katika nafasi 6,060 sawa na asilimia 49.35 ya nafasi hizo.

Amesema nafasi za mwenyekiti wa mtaa zinazogombewa ni 4,264 ambapo vyama 18 vya siasa viliweka wagombea katika nafasi 3,281 sawa na asilimia 76.94 ya nafasi hizo.

“Nafasi za mwenyekiti wa kitongoji zinazogombewa ni 63,886 ambapo vyama 18 vya siasa viliweka wagombea katika nafasi 21,636 sawa na asilimia 33.87 ya nafasi hizo,” amesema.

 Amesema nafasi zote zinazogombewa ni 80,430 (ukitoa nafasi za wajumbe wa serikali za vijiji na kamati za mitaa), ambazo zinajumuisha vijiji 12,280, mitaa 4,264 na vitongoji nafasi 63,886.

Waziri huyo amesema katika nafasi hizo zinazogombewam  vyama 18 vya siasa ukiacha CCM ambacho kimeweka wagombea katika nafasi zote, vyama hivyo vimeweka wagombea katika nafasi 30,977 kati ya nafasi 80,430 sawa na asilimia 38.51.

“Nimeona ni muhimu kuweka idadi hii wazi ili kuupa umma taarifa ya hali halisi ya uchukuaji wa fomu za kugombea nafasi mbalimbali kwa vyama vyote vya siasa hata kabla ya malalamiko ya kuenguliwa kinyume na taratibu,” amesema.

Waziri huyo amesema pamoja na kueleza takwimu hizo za ujumla ameona si vyema kukaa kimya na ni muhimu Watanzania wafahamu ukweli wa kilichofanyika au kilichotokea katika maeneo ambayo hayatajwi kabisa wala kuelezwa popote.

Waziri Mchengerwa amesema mtakumbuka yapo maeneo ambayo yalilalamikiwa kuhusu uteuzi wa wagombea na baadhi kuenguliwa kinyume cha kanuni.

“Nilisikia malalamiko hayo na nikatoa ufafanuzi juu ya hatua ambazo zinapaswa kuchukuliwa endapo kuna mgombea hakuridhika na mchakato wa uteuzi,” amesema.

Amesema baada ya kutoa siku za nyongeza za rufaa kuanzia Novemba 13-15, 2024 ili kuwahakikishia haki imekuwa ikitendeka na kanuni kufuatwa, wale wote ambao mapingamizi na rufaa zilizokidhi vigezo, wamerejeshwa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi.

“Taarifa nilizopokea kutoka katika halmashauri zote ni takribani kati ya rufaa 16,309 zilipokelewa baada ya muda wa nyongeza wa siku mbili ni rufaa 5,589 zilizokubaliwa. Hii ilizingatia dosari ambazo zilisababisha kutoteuliwa kwao hazikuwa kubwa zinazoweza kuathiri matokeo yaliyokusudiwa na kanuni,” amesema.

Nyongeza hiyo ya siku ilitokana na maombi ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi kumwomba Waziri Mchengerwa kuyapuuza makosa madogo madogo  kuenguliwa na warejeshwe ili kuleta ushindani katika uchaguzi huo utakaofanyika Novemba 27

Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa, Angelista Kihaga akijibu swali la uandikishaji ulivyokuwa, amesema uchaguzi huu ni wa ngazi za msingi kabisa ya makazi na unahusisha na wananchi wa eneo husika na hakukuwa na vizingiti vingi vya kuwafanya wananchi kutofahamiana.

“Kwa sababu hiyo, ndio maana wakati wa uandikishaji hakukuwa na masharti makubwa na wananchi wanaoandikisha, wanajuana,” amesema.

Katika uandikishaji huo, Waziri Mchengerwa alikwishasema waliojiandikisha kupiga kura siku hiyo ya uchaguzi ni milioni 31

Adai uchaguzi huu umefana

Akijibu swali aliloulizwa la tathimini yake kwa ujumla ya uchaguzi huo mpaka sasa,  amesema ni mzuri na unatoa funzo kwa kila mmoja kujipanga na kutambua umuhimu wa uchaguzi huo.

“Huu unakuwa uchaguzi wa kwanza kutokana na kuzungumzwa na matabaka yote. Natamani Watanzania waendelee kuzungumza na inatufunza katika chaguzi zijazo. Mwenendo huu umetusaidia Watanzania kujua umuhimu wa uchaguzi wa serikali za mitaa,” amesema.

Ikumbukwe makundi mbalimbali ya kijamii wakiwamo viongozi wa dini na wanasiasa wamekuwa wakikosoa mchakato wa uchaguzi huo, ikiwamo kuenguliwa kwa wagombea wa vyama vya upinzani.

Wito mkubwa wa makundi hayo umekuwa ni kuhakikisha uchaguzi huo unakuwa wa haki na huru.

Related Posts