WAZIRI KOMBO AAGANA NA BALOZI WA IRAN

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo ameagana na Balozi wa Jamhuri ya Kiislam ya Iran Mhe. Hossein Alvandi Bahineh ambaye amemaliza muda wake wa uwakilishi nchini.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika tarehe 15 Novemba,2024 katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam, Mhe. Waziri Kombo, amempongeza Mhe. Balozi Bahineh kwa kumaliza utumishi wake nchini na kumsihi akawe Balozi mzuri wa Tanzania nchini kwao.

Mhe. Waziri Kombo pia amempongeza Mhe Balozi Bahineh kwa kazi nzuri ya kuimarisha uhusiano na Ushirikiano Kati ya Tanzania na Iran ambayo ameifanya katika kipindi chake cha uwakilishi hapa nchini.

Amesema katika kipindi chake uhusiano Kati ya Tanzania na Iran umeendelea kuimarika na kutanua wigo wa maeneo ya ushirikiano Kati ya Tanzania na Iran.

Mhe. Waziri pia ameishukuru Iran kwa kuendelea kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kibiashara, na hivyo kuongeza mapato na kukuza uchumi wa Taifa.

Naye Balozi wa Iran Mhe. Bahineh ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.

Mhe. Balozi Bahineh amesema uhusiano kati ya Iran na Tanzania uliodumu kwa miaka 42, umesaidia mataifa hayo kukuza biashara na uchumi, na kuleta maendeleo kwa watu wake.

Balozi Bahineh amesema kupitia uhusiano mzuri wa kibiashara kati ya Iran na Tanzania , Iran imefanikiwa kukuza mapato yake kutoka Dola milioni 23 za Marekani hadi kufikia Dola milioni 99, kutokana na kukua kwa soko la bidhaa zake nchini.

Ameipongeza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kufanikisha Mkutano wa Tüme ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Iran (JPC), uliofanyika mwezi Oktoba 2024 jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa kufanyika kwa mkutano huo kumewezesha wafanyabiashara wa Tanzania na Iran kufanya vikao vya kibiashara na kisekta na kusaini Hati za makubaliano ya ushirikiano kwa utekelezaji.

Amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha uhusiano na Iran na kwa kuthamini mialiko ya viongozi kutembeleana, na kuongeza kuwa vitu hivyo vimesaidia kuimarisha uhusiano wa uwili kati ya nchi hizo.

Balozi Bahineh ameiomba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufungua Ofisi za Ubalozi nchini Iran ili kuimarisha na kuendelea kushirikishana zaidi na Iran.

Iran na Tanzania zinashirikiana katika maeneo ya kilimo, elimu, mifugo, maji, uwekezaji, nishati, madini, afya na ustawi wa jamii.




Related Posts