Dar es Salaam. Chama cha ACT- Wazalendo, kwa mara ya kwanza kimekuja na ilani yake ya uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji yenye mambo tisa yatakayosimamiwa na kutekelezwa na viongozi wao watakaochaguliwa katika uchaguzi utakaofanyika Jumatano ya Novemba 27, 2024.
Miongoni mwa mambo hayo ni kutoa viongozi waaminifu, jasiri na mahiri katika vijiji, mitaa na vitongoji, kurejesha nguvu za serikali za mitaa kwa wananchi, kuboresha huduma za jamii kwa wote mijini na vijijini.
Pia kuwahudumia wananchi kwa kutoa huduma bora na stahiki, kusikiliza changamoto zao kwa ukaribu, kupambana na ufisadi, kuhakikisha kila fedha inayokusanywa inatumika kuondoa umaskini vijijini, kuondoa vitisho, ubabe na uonevu kwa wananchi mijini na vijijini.
Akiizindua ilani hiyo leo Jumapili Novemba 17, 2024, Kiongozi wa ACT- Wazalendo, Dorothy Semu amewataka Watanzania kutumia kura yao kufanya mabadiliko, akisema ahadi ya chama hicho ni kuwajibika, kutoa huduma bora na kujenga mitaa, vijiji na vitongoji vinavyostawi.
Uzinduzi wa ilani hiyo uliofanyika makao makuu ofisi za chama hicho, Magomeni jijini Dar es Salaam na umehudhuriwa na kiongozi wa zamani wa chama hicho, Zitto Kabwe, wadau wa demokrasia, asasi za kiraia pamoja na wagombea wa uenyekiti wa vijiji, mitaa na vitongoji kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Akichambua maeneo hayo, Semu amesema chama hicho kikishika mitaa, vijiji na vitongoji kitapiga marufuku michango ya mitihani shuleni, masomo ya ziada, ulinzi na badala yake kitasimamia matumizi sahihi ya ruzuku inayotolewa na Serikali kuu.
“Tutatenga asilimia mbili ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa ajili ya lishe na chakula shuleni ili kukabiliana na changamoto ya udumavu na utoro. Tutajenga shule shikizi kwa maeneo yaliyo mbali na shule ili kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na shule iliyo karibu na wananchi,” amesema Semu.
Amesema wamedhamiria kupambana na rushwa, ufisadi, ubadhirifu wa fedha za umma, sambamba na kuimarisha miundombinu vijijini ili kuamsha uchumi, kuzalisha ajira na kuondoa umasikini.
“Ili kuwa na viongozi watakaopambana na rushwa, ubadhirifu na ufisadi tutahakikisha fedha na rasilimali za umma zinatumika kuboresha maisha ya watu wote,” amesema Semu.
Katika kufanikisha hilo, Semu amesema ACT- Wazalendo, itawafukuza uanachama, kuwachukulia hatua nyingine za kisheria viongozi wa kuchaguliwa watakaojihusisha na vitendo vya rushwa na ubadhilifu.
“Itawachukulia hatua za kisheria watumishi wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa na ubadhirifu. Tutapiga marufuku utaratibu wa wananchi kulipishwa fedha kwa ajili ya fomu, barua ya utambulisho, mihuri katika ofisi za serikali za mitaa na vijiji,” amesema Semu.
Ameongeza, “tumedhamiria kujenga uwezo wa kujitegemea wa serikali za mitaa, lakini pia kujenga mitaa na vijiji salama kwa watu kufanya biashara zao bila bughudha ya migambo, polisi wala sungusungu.
Amesema chama hicho kitasimamia viongozi na watumishi wa Serikali kuzingatia misingi ya haki na uwajibikaji, uaminifu na wenye uwezo wa kusimamia utekelezaji bora wa miradi ya maendeleo na masilahi ya wananchi.
“Itarejesha na kuimarisha nguvu na sauti ya umma kwenye mikutano ya mtaa na vijiji na kuhakikisha mikutano inafanyika kwa uwazi na kwa mujibu wa sheria. Itavijengea uwezo vyombo vya uwakilishi wa wananchi, kama baraza la madiwani, baraza la maendeleo ya kata na halmashauri za vijiji,” amesema Semu.
Naye, Zitto amesema wanaouchukulia uchaguzi wa serikali za mitaa kama chaguzi zingine ukiwamo uchaguzi mkuu unaokuwa na ilani ya miaka mitano, ndio maana wameamua kuja na ilani hiyo kwa mara ya kwanza.
“Tunaposema huduma zitatolewa bila malipo kwenye ofisi za serikali za mitaa, vijiji na vitongoji tunamaanisha, tukipata taarifa ya mwenyekiti kijiji au mtaa anayewatoza wananchi fedha kwa huduma ambazo tumesema bure tutamfukuza.”
“Tutamfukuza ili akatafute chama cha kugombea ili kudhulumu watu, sijui tumeelewana vizuri, kwa hiyo haya maelekezo yaliyowekwa kwenye ilani yachukuliwe kwa uzito mkubwa na kutumika vizuri kwenye kampeni ili tuongoze kwa tofauti,” amesema Zitto.
Zitto amefafanua maeneo machache waliopata nafasi ya kusimamisha wagombea yawe mfano wa namna chama hicho, kitakavyoongoza serikali endapo kitashinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
“Kama wewe umeshinda kwenye mtaa, jichukulie ndio rais wa ACT ungependa kuongoza vipi nchi, ndio uongoze mtaa kwa namna hiyo,” amesema Zitto ambaye ni mbunge wa zamani wa majimbo ya Kigoma Kaskazini na Mjini.
Kwa mujibu wa Zitto, ACT- Wazalendo imejiandaa na uchaguzi huo, ndio maana tangu mwaka 2022 viongozi wakuu wamekuwa wakifanya ziara maeneo ya vijiji kwa ajili ya maandalizi ya mchakato huo.
“Hatukujiandaa kisiasa bali mawazo ya kwenda kwa wananchi, ndicho tulichokifanya leo kuzindua ilani ya uchaguzi wa serikali za mitaa,” amesema Zitto.
Baadhi ya wagombea uenyekiti wa serikali mitaa, vijiji na vitongoji waliohudhuria uzinduzi huo, wamefurahishwa namna ilani ilivyogusa mambo ya msingi ikiwemo matatizo ya rushwa, migogoro ya ardhi na huduma za jamii.
“Endapo nitaibuka kidedea nitahakikisha wananchi hawatozwi fedha za malipo ya fomu za barua za utambulisho, badala yake watapewa huduma bure,” amesema Matrida Francis anayetokea wilayani Kilombero Mkoa wa Morogoro.