Dar es Salaam. Wachumi, wafanyabiashara na wamiliki wa malori nchini wameeleza mategemeo yao ya kuanza kwa usafirishaji wa mizigo kwa reli ya treni ya kisasa (SGR) mwakani, wakiamini utarahisisha biashara kufanyika haraka na kupunguza gharama za bidhaa.
Kwa nyakati tofauti walisema usafiri wa reli ni wa uhakika katika usafirishaji wa mizigo.
Faida nyingine ya usafirishaji mizigo kwa njia ya treni ni kuepuka foleni inayochangiwa na malori barabarani, kumuwezesha mkulima kuuza mazao yake katika masoko anayohitaji kwa haraka bila kupitia kwa madalali.
Akizungumzia hilo hivi karibuni alipozungumza na Mwananchi, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads), Mohamed Besta amesema ukarabati wa barabara pia ni kazi endelevu.
“Matengenezo ya barabara ni endelevu hasa kwa zile zilizojengwa kwa lami iwe inatumika au haitumiki, itazeeka na kuharibika yenyewe kutokana na mabadiliko ya kikemikali,”amesema Besta.
Besta amesema huduma ya barabara na reli zinategemeana katika kukuza uchumi na kuongeza kuwa kutokana na ongezeko la mizigo, hawategemei malori kupungua katika matumizi ya barabara.
Hata hivyo, uzoefu unaonyesha tofauti katika njia ya Dar es Salaam – Dodoma ambako safari za abiria za SGR zinatolewa, chaguo la wengi sasa ni treni kuliko mabasi.
Kwa mujibu wa TRC, treni ya SGR itakuwa na uwezo wa kubeba mpaka tani 10,000 za mzigo kwa mkupuo sawa na uwezo wa malori 500 ya mizigo.
Taarifa ya kuanza kazi kwa treni ya mizigo ilitolewa mwishoni mwa juma na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Augustine Vuma.
Akiwa kwenye ziara ya Kamati ya PIC iliyofika Shirika la Reli Tanzania (TRC) kupokea taarifa ya utekelezaji wa mradi wa SGR, Vuma alisema shirika hilo limewaeleza wataanza kusafirisha mizigo kwa njia ya reli kuanzia Januari au Februari.
“Maana yake hapa tunategemea mapato yataongezeka zaidi ya mara tatu,”alisema.
Kauli hiyo ilifuatiwa na taarifa kwa umma iliyotolewa jana na TRC ikisainiwa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano Fredy Mwanjala ikisema, utengenezaji wa mabehewa 264 ya mizigo China umekamilika na yataletwa nchini Desemba 2024.
Mabehewa hayo 264 ni sehemu ya mabehewa 1,430 yaliyopaswa kutengenezwa na Kampuni ya CRRC kwa mujibu wa mkataba.
“Meli iliyobeba mabehewa hayo imeng’oa nanga nchini China Novemba 12, 2024, katika mzigo huo kuna mabehewa 200 ya kubeba makasha (makontena) na mabehewa 64 ya kubeba mizigo isiyofungwa,”inaeleza taarifa hiyo.
Mategemeo kuanza reli ya mizigo
Kutokana na kauli hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori nchini (TAMSTOA) Chuki Shaban amesema hakuna athari watakayoipata kwa kuanza kazi treni ya mizigo akisema kila mbuzi atakula kwa urefu wa kamba yake.
Shaban alisema uzuri wa lori linafika kila sehemu, “umuhimu wa malori uko pale pale hata Ulaya bado yapo na yanafanya kazi, tuna wanachama 26,000 nchi nzima na sekta yetu ni kubwa kwa maana hiyo uchumi tunauchangia kwa kiwango kikubwa.”
Hofu ya ajira zao kutikishwa na usafirishaji wa mizigo kwa njia ya reli alisema ni jambo lisilowezekana kwa kuwa anayeongoza treni ni mmoja.
Amani Munuo, mfanyabiashara jijini Dar es Salaam amesema katika biashara, miundombinu ya usafirishaji ni muhimu.
“Usafiri huu unachukua mizigo mingi kwa wakati mmoja na ni nafuu ikilinganishwa na usafiri mwingine kwahiyo kwa mfanyabiashara ni faida kuliwahi soko anapokuwa na bidhaa zake,”amesema.
Mchambuzi wa uchumi, Profesa Abel Kinyondo amesema mapato ya shirika lolote la reli kwa asilimia 80 yanatokana na usafirishaji wa mizigo na sio abiria.
“Kama TRC itaanza kusafirisha mizigo maana yake tunakwenda vizuri, mizigo itasafirishwa kwa wingi na haraka kwasababu kwa sasa hakuna usafiri unaosafirisha mizigo kwa haraka hapa nchini,”amesema.
Amesema kuanza kwa usafiri wa mizigo kwa njia ya reli ni hatua ya kufurahiwa kwa kuwa, masoko makubwa yatafikiwa kwa urahisi.
Manufaa anayotaja Profesa Kinyondo yatawagusa moja kwa moja wakulima ambao watakuwa na uwezo wa kusafirisha mizigo yao nje ya shamba lake na kupata bei kubwa katika masoko anayohitaji kwa haraka.
“Usafiri huu utawafanya wakulima kuwaepuka madalali kwenye mazao yao, usafiri huu una uwezo wa kumtoa mkulima kwenye umasikini maana unamuwezesha kuuza mazao kwa bei nzuri,”amesema.
Faida nyingine ya kuanza kwa usafiri huo, Profesa Kinyondo amesema ni kupunguza msongamano wa foleni barabarani.
Kuondolewa kwa foleni barabarani inayosababishwa na malori ya mizigo ndiko Profesa Kinyondo anatafsiri kutasaidia barabara kuwa na umri mrefu na uchumi utaimarika.
Hata hivyo, faida nyingine ni usafiri wa abiria kuwa wa haraka kutokana na foleni kupungua ambao ulichangiwa na msongamano wa malori ya mizigo.
Kwa wamiliki wa malori, Profesa Kinyondo amesema usafiri wa treni unakwenda kupunguza malori barabarani na ndio mwanya wa magari hayo kuelekea maeneo yasiyo na usafiri.
“Katika eneo ambalo kutatokea mabadiliko magari hayo yanaweza yakawa machache au yakahamishiwa upande mwingine, yatakwenda kushindana na hii ni faida kwasababu maeneo mengine usafiri ni shida,”amesema.
Mchambuzi mwingine, Dk Yohana Lawi wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) amesema kusafirisha mizigo kwa njia ya reli faida yake ni kubwa ikiwamo kwa haraka na gharama nafuu.
“Unakwenda kupunguza gharama za usafirishaji wa bidhaa maana yake mwananchi wa kawaida anakwenda kupata bidhaa kwa gharama nafuu, usafiri pia ni rafiki wa mazingira hivyo hakutakuwa na hewa ya ukaa ambayo inachangia ongezeko la joto duniani,” amesema.
Faida nyingine, Dk Lawi amesema barabara zitakuwa salama kutokana na malori mengi kuwa na mchango mkubwa katika uchakavu wa barabara.
Kwa upande wa fedha za kigeni, amesema ule uhaba ambao umekuwa ukishuhudiwa hautaathiri eneo la usafirishaji kwa kuwa katika usafirishaji kwa njia ya treni fedha za ndani ndizo zitatumika zaidi.
Shabani Ali, mkazi wa Mabibo Dar es Salaam, amesema ujio wa treni utasaidia gharama za maisha kushuka.
“Gharama za bidhaa zinakuwa kubwa kutokana na gharama za usafiri kuwa juu, tunapokwenda kutumia treni ya mizigo sio tu usafiri unakuwa rahisi bali gharama za maisha zinapungua na uchumi wa mtu mmoja mmoja unaimarika,” amesema.