BARAZA LA MADIWANI WILAYA YA SAME LAAZIMIA KUMUONDOA BIBI AFYA KATA YA HEDARU

 

Na Ashrack Miraji App 

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Same limeazimia kumuondoa kazini Hellen Sige, aliyekuwa Bibi Afya wa Kata ya Hedaru, kwa tuhuma za kugushi vyeti. Uamuzi huo ulifikiwa mwishoni mwa wiki hii katika kikao cha kawaida cha baraza.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Yusto Mapande, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Msindo, alithibitisha hatua hiyo na kumpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri, Jimson Mhagama, kwa utekelezaji wa makubaliano ya kuondoka kwa mtumishi huyo. Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuboresha mifumo ya kidijitali kwa kutoa vishikwambi kwa Madiwani ili kurahisisha utoaji wa taarifa na kuongeza ufanisi wa utendaji

Mkuu wa Wilaya ya Same, Kaslida Mgeni, alitumia kikao hicho kuipongeza Halmashauri kwa usimamizi mzuri wa mapato na miradi ya maendeleo. Aliwashukuru Madiwani na watumishi wa umma kwa juhudi zao, akieleza kuwa Wilaya ya Same imekuwa mfano mzuri katika ukusanyaji wa mapato mkoani Kilimanjaro.

“Ni jambo la kujivunia kuona ushirikiano mkubwa kati ya Madiwani na watumishi wa umma. Hili linaonyesha juhudi zenu za kusimamia miradi ya maendeleo. Serikali ya Wilaya yetu imepata zaidi ya bilioni 58 kwa ajili ya miradi ya maendeleo kupitia msaada wa Rais, na ni muhimu taarifa kuhusu maendeleo hayo ziendelee kuwafikia wananchi,” alisema Mkuu wa Wilaya.

Mkuu wa Wilaya alihimiza Madiwani na wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, akisisitiza kuwa uchaguzi huo ni sehemu muhimu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu.

“Tunahitaji mshikamano na heshima katika kampeni. Serikali imeleta mabadiliko makubwa kwa maendeleo, na ni jukumu letu kuhakikisha mafanikio haya yanaendelezwa kwa kuimarisha uongozi wa Serikali za Mitaa,” alisema.

Aidha, Mkuu wa Wilaya aliwataka Madiwani kuendelea kusimamia kwa karibu miradi ya maendeleo katika kata zao. Alisisitiza kuwa changamoto zinapojitokeza ni muhimu kushirikiana kwa ajili ya kutafuta suluhisho kwa ustawi wa wananchi.

“Tutakapokuwa na mshikamano thabiti, tutafanikisha malengo yetu ya kuboresha maisha ya wananchi. Kazi yenu ni kubwa, lakini kwa kushirikiana, tunaweza kufanikisha maendeleo ya Wilaya yetu,” alisema.

 

Related Posts