Benki ya Akiba yawatoa hofu wateja wake Kariakoo

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Benki ya Akiba (ACB) imewaomba wateja wake walioathirika na janga la kuporomoka gorofa Kariakoo kufika kwenye matawi kutoa taarifa za athari walizopata.

Kauli hiyo imetolewa leo Novemba 17,2024 na Kaimu Ofisa Biashara Mkuu wa benki hiyo, Dk. Danford Muyango, wakati benki hiyo ilipofika katika eneo la Karikoo kutoa pole na kuwapa msaada waathirika.

Amesema benki hiyo itatoa usaidizi wa tathmini wa kina kuhusu huduma za bima na kuanzisha utaratibu wa marejesho ya mikopo yao kulingana na hali zao.

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Tobha Nguvira ambaye pia ni msimamizi wa kitengo cha maafa mkoani humo, ameipongeza benki hiyo kwa kuendelea kuhudumia wateja wake pamoja na kushiriki katika juhudi za kijamii wakati wa dharura na majanga, ikiwa ni sehemu ya dhamira yake ya kujenga jamii imara na yenye mshikamano.

“Tunashukuru Benki ya Akiba imetoa msaada wa maji ya kunywa kusaidia timu ya uokozi inayofanya juhudi kubwa za kuokoa watu waliokumbwa na ajali mbaya na ya kusikitisha.

“Hii ni sehemu ya dhamira yake ya kujenga jamii imara na yenye mshikamano,” amesema Dk. Nguvira.

Ujumbe wa benki hiyo uliongozwa na wafanyakazi wa matawi ya Kariakoo pamoja na makao makuu akiwemo Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano, Dora Saria, na Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji, Dk. Danford Muyango.

Related Posts