Siha. Wanafunzi wa Shule ya Msingi Lemosho, Kata ya Indumet, wilayani Siha mkoani Kilimanjaro, wako katika hatarini kupata magonjwa ya mlipuko, ikiwamo kipindupindu na UTI, kutokana na ukosefu wa majisafi na salama shuleni hapo.
Tatizo hilo linadaiwa ni kutokana na kukatwa kwa huduma ya maji na Bodi ya Maji ya Magadini Makiwaru wakidai deni la zaidi ya Sh1 milioni.
Hata hivyo, mwalimu mkuu wa shule hiyo, Raymond Lengereri akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Novemba 17, 2024, amesema huduma ya maji ipo na haijakatwa kama inavyodaiwa.
“Ingawa ni kweli tunadaiwa bili ya maji na mamlaka,” amesema mwalimu huyo.
Akizungumzia hilo, diwani wa kata hiyo, Vincent Kileo amesema shule inadaiwa bili ya maji lakini juhudi zinaendelea za kulilipa deni hilo.
“Kwa sasa shule inatumia maji ya mfereji, hii changamoto ya bili ya maji ya bomba inaendelea kuathiri wanafunzi, kwa sababu shule nyingi zinashindwa kulipa gharama za awali za maji,” amesema Diwani Kileo.
Ezekiel Maningo kutoka Bodi ya Magadini Makiwaru, amesema taasisi zinazodaiwa zinapaswa kufika ofisini kwa utaratibu wa kusuluhisha changamoto hizo.
Wadau wa elimu wameitaka Serikali kuchukua hatua ya kuchimba visima kwa shule ili kuepusha changamoto kama hizo zinazohatarisha afya za wanafunzi.
Akizungumzia adha hiyo, mwanafunzi wa shule hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Ernest Shirima mkazi wa Indumet, amesema huduma ya maji ya bomba ilikatwa tangu tangu Juni, mwaka huu. Amesema hali hiyo imewasababishia kutumia maji kidogo sana wakienda kujisaidia katika vyoo vipya vya kisasa vilivyojengwa shuleni.
“Hivi vyoo vinahitaji maji mengi mtu akitumia, sasa hayatoki yamekatwa, tunatumia maji kidogo kwa sababu hatuna uhakika wa kupata maji,” amesema mwanafunzi huyo.
Hata hivyo, mwanafunzi huyo ameiomba Serikali izungumze na uongozi wa shule na wa Bodi ya Magadini ili maji yarejeshwe.
Naye mkazi wa Matadi, Anna Judika amesema wanafunzi sasa wanalazimika kunywa maji ya mfereji, ambayo si salama, baada ya kukosekana maji ya bomba.
Amewaomba wazazi na jamii kushirikiana kutafuta suluhisho ili kulinda afya za watoto wao dhidi ya magonjwa yanayotokana na ukosefu wa maji safi.
Idrisa Mndeme, mdau wa elimu wilayani humo, ametoa wito kwa Serikali kusaidia kuchimba visima katika shule za msingi ili kuhakikisha upatikanaji wa maji wa kudumu.
“Ni muhimu kwa kila shule kuwa na kisima cha maji ili kuepusha changamoto zinazojitokeza mara kwa mara na kulinda afya za wanafunzi,” amesema.
Mndeme amesema tatizo la uosefu wa maji linaathiri usafi na ustawi wa shule nyingi, licha ya juhudi za Serikali kujenga shule bora.
Mndeme ameiomba pia Serikali kuwekeza zaidi kwenye miundombinu ya maji ili kuhakikisha changamoto hiyo inatatuliwa kwa manufaa ya wanafunzi na jamii kwa jumla.