Bima ya Sh130 milioni ilivyotumika kuokoa maisha ya watoto njiti

Dar es Salaam. Kufikiria kuuza ogani yake ya figo, nyumba na hata kujiua ni miongoni mwa suluhu zilizopita kichwani mwa Beatrice Mbawala, Februari 2018, alipojifungua watoto wanne kabla ya wakati ‘njiti’ katika Hospitali ya Aga Khan.

Beatrice ambaye ni Ofisa Tarafa wa Kibamba, wilayani Ubungo, Dar es Salaam  amesema upasuaji wake na matibabu pamoja na gharama za matibabu ya watoto mpaka wanafikisha umri wa miaka mitano zililipwa kupitia Bima ya NSSF ambayo pia ni ofisi anayofanya kazi mumewe gharama zinazofikia Sh130 milioni.

Bitrice ambaye amebaki na watoto watatu wenye umri wa miaka sita, ni miongoni mwa maelfu ya wake kwa waume nchini Tanzania, wanaotumia mamilioni ya fedha kuokoa uhai wa watoto waliozaliwa kabla ya wakati.

Chapisho jipya lililozinduliwa jana Jumamosi, Novemba 16, 2024 linaonyesha Sh1.3 milioni hutumika kama gharama kwa kila mtoto njiti mmoja anayezaliwa, ambayo ni sawa na Sh19,877 kwa siku kwa kipindi cha miezi miwili hadi mitatu mama anapokuwa hospitalini kwa uangalizi.

Akisimulia, Beatrice anasema alikwenda hospitali kwa ajili ya kliniki ya mwezi pamoja na kuchoma sindano ya kukomaza mapafu ya watoto, lakini baada ya vipimo ilionyesha anatakiwa kujifungua haraka mimba ikiwa na miezi saba.

“Mtoto mkubwa alitoka na uzito wa kilo moja na gramu 400 na mdogo alitoka na uzito wa kilo moja na gramu 300. Nilipoambiwa hongera umepata watoto wakubwa nilidhani watakuwa wakubwa kweli. Nimeenda kuwaona naona wadogo kama panya hawana macho, masikio huyaoni hawana hata nywele niliogopa, niliona si wa kwangu,” amesimulia.

Beatrice anasema alikaa miezi miwili na nusu Hospitali ya Aga Khan, akiwa halali, haogi vizuri kutokana na msongo na alisahau kupaka mafuta.

“Nilikaa miezi miwili na nusu nikiwa Aga Khan, baadaye niliruhusiwa watoto wawili wakiwa wa kike na wawili wa kiume. Nikiwa nyumbani walianza kuugua nilirudi mara kwa mara hospitali, kuna nyakati nilidhani hakutakucha nitampoteza mtoto yeyote kati yao, walilazwa ICU mara kwa mara.

“Nikiwa huko nilikata tamaa na safari hii nilitaka kujiua. Bahati nzuri nikakutana na dada mmoja anaitwa Radhia akanipa ushuhuda kwamba watoto njiti wanakua. Nikaona huyu ndiyo mwenzangu na hapo nikawa kesho yangu inaweza kuwa rahisi.

“Niliruhusiwa na kurudi nyumbani. Lakini baada ya wiki chache watoto wangu wakaanza kuumwa mafua na ikasogea na kuwa nimonia kwa wote wanne, nilirudi hospitali na kulazwa tena ICU wiki tatu na walipokuwa sawa watatu niliambiwa nirudi nyumbani mmoja nimuache.”

Beatrice anasema alimuacha mmoja na baada ya siku moja alifariki, akabaki na watoto watatu,“ninazika huyu mmoja watatu wakaanza tena kuumwa hoi tukarudi hospitali. Huko mmoja nikaambiwa figo zimefeli na hawezi tena kuishi, nilipiga moyo konde nikaanza kutangaza kuuza figo yangu.”

Anasema kwa kipindi chote upasuaji wake na matibabu pamoja na gharama za watoto walitibiwa kupitia ofisi anayofanya kazi baba yao NSSF gharama zinazofikia Sh130 milioni.

Hata hivyo, alipoambiwa mwanaye ana shida ya figo alifikiria kuuza nyumba yenye thamani ya zaidi ya Sh100 milioni kwa bei rahisi kwa kuwa wakati huo bima isingelipia matibabu ya nje ya nchi.

“Nilimwambia daktari akifa huyu na mimi nimekufa, alinipa moyo lakini bado nilikuwa na fikra hasi. Nikataka kuuza nyumba kwa Sh20 milioni. Baadaye tukashauriana na mume wangu hatukuiuza, tulikuwa na akiba ya Sh7 milioni na kazini kwake wakachanga zaidi ya Sh10 milioni na bosi wake akampatia Sh10 milioni. Rafiki yangu akanichangia Sh10 milioni na fedha zingine tulizipata kwa wahisani tukaona tumpeleke Aga Khan ya Nairobi, Kenya. 

“Kufika huko wawili waliokuwa wazima ndiyo wakalazwa tulilazimika kukaa kwa zaidi ya wiki tatu tukiwauguza na huyu aliyekuwa hoi Mungu alimponya naamini hivyo mpaka kesho kule walisema hana changamoto na alirudi sawa.”

Beatrice anasema licha ya changamoto za makuzi ya njiti hapo wasichana wa kazi walimsumbua zaidi, ilifika hatua alikuwa na wafanyakazi watano.

“Kuna nyakati waliamka asubuhi wote wanaaga wanaondoka. Walinisumbua sana mpaka nikampata mmoja kutoka Kenya pamoja na mdogo wangu walionilelea hawa watoto mpaka sasa wana umri wa miaka sita na wanasoma darasa la kwanza,” anasema Beatrice.

Saada Nassor (42) ni miongoni mwa wanawake waliopitia uchungu mkubwa na kupoteza kazi na fedha nyingi kutunza mtoto wake wa kwanza njiti mwaka 2017.

“Muhimbili ilinipa uzoefu sana, katika familia hakukuwa na mtoto njiti sikuwahi kuona nilikuwa nasikia tu. Alizaliwa kabla ya siku na matatizo, uti wa mgongo ulikuwa haujashikana, alikuwa na tundu mbili kwenye moyo, sehemu za siri mirija hakuna.

“Gharama ilikuwa kubwa sana, niliacha kazi na biashara zangu zote nashukuru mume alikuwa upande wangu. Sasa ana miaka saba, hakuna uzoefu wa mtoto njiti. Nilimlea kwa gharama za kulipia kitanda Sh82,000 kila siku na mtoto analipia, changamoto ya kwanza gharama, muda wa kupumzika sikupata kila masaa matatu unaenda kukamua maziwa,” anasema Saada.

Nora Michael anasema kwa kuwa alijifungua akiwa kibarua, alishindwa kupata stahiki zozote na gharama ilifikia Sh4 milioni Muhimbili na baada ya kushindwa kulipia alikaa wiki tatu hospitalini licha ya kuruhusiwa mpaka alipopewa msamaha.

Mary Marwa ni miongoni mwa wanawake waliopoteza ajira zao, baada ya mimba aliyokuwa akitolewa yenye miezi mitano kugeuka mtoto.

“Changamoto za kiafya ziliwalazimu madaktari waitoe mimba ikiwa na miezi mitano, mama akiwa ametolewa waliamini ile nyumba ya mtoto hayuko hai. Muuguzi badala ya kwenda kutupa sehemu wanayochoma moto alisita baada ya kuona ule mfuko unachezacheza.

“Mimba ilikuwa na wiki 20. Akaona hapana acha nifungue akaona mtoto mzima akamchukua na kumhifadhi pembeni kabla ya kuita madaktari ambao walimchukua na kumpa huduma. Mama alipoamka wanamwonyesha alikataa maana mtoto alikuwa kama mjusi, lakini sasa Aron yupo chekechekea,” anasimulia Dk Sylivia Ruambo.

Mkurugenzi wa Doris Mollel Foundation, Doris Mollel anasema utafiti ulioanza kufanyika mwishoni mwa mwaka 2022 umebaini kinamama wengi husitisha kazi zao kwa muda mrefu huku familia ikilazimika kutumia zaidi ya kiwango hicho cha fedha.

“Utafiti huu umefanywa na Chama cha Madaktari Tanzania kwa kushirikiana na daktari bingwa wa magonjwa ya watoto wachanga kitengo cha watoto njiti Muhimbili Dk Robert Moshiro na Mkuu wa kitengo cha watoto njiti Dodoma Dk Albert Chotta,” anasema.

Doris anasema utafiti huo uliofanywa kwa wanawake 406 waliojifungua kabla ya wakati, unaonyesha gharama hizo si za kitabibu pekee, kwani kuna gharama zaidi ya hizo ambazo hutokana na mahitaji mbalimbali katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo.

Hata hivyo, anasema tangu kuanzishwa kwa taasisi yake, wameshachangia katika vituo 85 kote nchini, huku wakigawa vifaa vyenye thamani ya Sh1.5 bilioni.

Akielezea changamoto za kujifungua kabla ya wakati, Dk Chotta anasema baadhi ya sehemu za mfumo wa mtoto, neva zinakuwa hazijakua vyema.

“Watoto hawa wana kiwango kidogo cha mafuta ya ngozi, hawachezi na nyakati zingine husahau kupumua mpaka umshtue ndiyo anaendelea kupumua. Watoto hawa wana mapafu ambayo hayajakomaa, hivyo wana matatizo ya kupumua, hawana kingamwili imara, hivyo wako katika hatari kuu zaidi ya kuambukizwa.

“Vena za ubongo wao ni nyembamba na hazijapevuka, hivyo zinaweza kuvuja damu kwa urahisi, hatushauri mzazi kumtikisa kabisa. Pia, ni dhaifu sana wanalishwa kidogo na kwa kipimo mama akikosea tu utumbo wao unaoza tunapoteza,” anasema Dk Chotta.

Related Posts