MSHAMBULIAJI wa Songea United, Andrew Chamungu amesema msimu huu umekuwa ni mgumu kwake kutokana na kutopata nafasi ya kucheza mara kwa mara ndani ya kikosi hicho, ingawa hajakata tamaa na ataendelea kupambana kushawishi benchi la ufundi.
Nyota huyo aliyefunga mabao matatu ya Ligi ya Championship hadi sasa, amekuwa akipigwa benchi na washambuliaji, Cyprian Kipenye na Ramadhan Kipalamoto ambao kila mmoja wao amefunga mabao manne kati ya 12 yaliyofungwa na kikosi hicho kizima.
“Msimu umekuwa mgumu kwa sababu ushindani umekuwa mkubwa na kila mmoja wetu anapambana kadri ya uwezo wake, hii kwangu ni njia ya kuniamsha na kunipa morali ya kufanya vizuri na kurudisha imani kwa mashabiki zangu zaidi ya msimu uliopita.”
Chamungu aliyewahi kutamba na timu mbalimbali zikiwemo, Polisi Tanzania, Mbuni na Kitayosce ambayo kwa sasa ni Tabora United, alisema ushindani uliopo kikosini humo unampa ari ya kupambana na kuacha kubweteka tofauti na msimu uliopita.
Msimu uliopita nyota huyo alifunga mabao 10 akiwa na kikosi hicho ambacho zamani kilikuwa kikifahamika kwa jina la FGA Talents FC, nyuma ya aliyekuwa mshambuliaji wa KenGold anayeichezea Fountain Gate kwa sasa, Edgar William aliyefunga 21.