Sumbawanga. Mahakama ya Rufani, imemfutia kifungo cha miaka 30 jela, alichoadhibiwa mchezeshaji musiki (DJ), Sokolo Richard kwa kosa la kumpa mimba mwanafunzi wa kidato cha pili na kumhukumu kifungo cha miaka mitano jela.
Baada ya mwanafunzi huyo kumtaarifu DJ kuwa ana ujauzito wake, alimtaka asimtaje lakini akaendelea kulea mimba hiyo na hiyo ni moja ya sababu ya kumpunguzia kifungo lakini pia kwa sababu ni mkosaji wa mara ya kwanza.
Katika hukumu yao waliyoitoa Novemba 15, 2024, jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani Tanzania waliosikiliza rufaa hiyo, wamebariki kutiwa kwake hatiani.
Hata hivyo, majaji hao, Barke Sehel, Dk Paul Kihwelo na Gerson Mdemu walisema Mahakama ya Wilaya ya Sumbawanga iliyompa adhabu ya kifungo cha miaka 30 iliegemea kanuni isiyo sahihi katika kufikia hitimisho la kumhukumu adhabu hiyo.
Walisema adhabu ya kifungo cha miaka 30 inayotajwa katika kifungu cha 60A(3) cha Sheria ya Elimu sio cha lazima, bali Mahakama ina utashi katika kutoa adhabu ya kifungo kwa kuegemea mazingira ya kesi na kujutia kosa hilo.
“Kwa mazingira ya rufaa hii, mrufani alikuwa ni mkosaji wa kwanza na kwa kweli alikuwa akitunza kiumbe ambacho kilikuwa hakijazaliwa. Tunakubaliana na wakili wa Serikali kuwa kifungo kilikuwa kikubwa na hakikuzingatia kanuni,”walisema.
“Hivyo, tuna kila sababu ya kuingilia kifungo hicho haramu alichopewa na tunatumia mamlaka tuliyonayo kukifuta kifungo cha miaka 30 na badala yake atatumikia kifungo cha miaka mitano jela kuanzia siku alipokamatwa.”
Namna alivyomjaza mimba mwanafunzi
Katika hati ya mashitaka, inaelezwa kuwa kati ya Februari 1 na 28, 2018, huko Kijiji cha Kasokola Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi, DJ huyo alimpa mimba mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kasokola kinyume cha Sheria ya Elimu.
Ushahidi ulieleza kuwa mwathirika huyo alikuwa alijiunga na kidato cha kwanza mwaka 2017 na alipata ujauzito akiwa kidato cha pili na baada ya kupata ujauzito huo, kiwango cha kitaaluma cha mwanafunzi huyo kilianza kuporomoka.
Taarifa zikaeleza kuwa, mwanafunzi huyo alikuwa akionekana katika nyumba ya mama Mindys na alikuwa akikutana mara kwa mara na DJ huyo na mazingira hayo yalimfanya awe mshukiwa wa kwanza wa ujauzito huo.
Baada ya mwanafunzi huyo kubanwa, alimtaja Sokolo Richard kuwa ndiye mhusika wa ujauzito huo na baadaye ya kupelekwa Hospitali ya Serikali ya Mpanda na kufanyiwa vipimo, alibainika kuwa na ujauzito wenye umri wa miezi minane.
DJ huyo alikamatwa na polisi Septemba 25,2018 na katika mahojiano polisi, alikiri kuwa na uhusiano ya kimapenzi na mwanafunzi huyo lakini alipofikishwa mahakamani alikana kuhusika japo alikiri kumfahamu mwanafunzi huyo.
Ni kutokana na ushahidi wa mashahidi watano akiwamo mwathirika, daktari, wazazi, polisi na mkuu wa Shule ya Kasokola, DJ huyo alitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kumjaza mimba mwanafunzi huyo.
Mashahidi hao walisema mrufani huyo alimpeleka mwanafunzi huyo akaishi na wazazi wa mrufani ili asiweze kutokea mahakamani kutoa ushahidi lakini mwathirika alisimama na msimamo ndiye mhusika wa ujauzito huo.
Katika maelezo yake polisi, mwanafunzi huyo alieleza kuwa walianza uhusiano wa kimapenzi na mrufani mwaka 2018 na hajawahi kuwa rafiki mwingine wa kiume na walikuwa wakifanya mapenzi porini na mrufani.
Hakuridhika na hukumu hiyo akakata rufaa katika Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, iliyokubaliana na kile ambacho Mahakama ya Wilaya ilikiamua, hakuridhika akaamua kukimbilia Mahakama ya Rufani Tanzania.