Arusha. Mahakama ya Rufani, imebatilisha mwenendo wa kesi na kufuta hukumu ya adhabu ya kunyongwa hadi kufa waliyokuwa wamehukumiwa wakazi wanne wa Sumbawanga mkoani Rukwa, baada ya kubaini kasoro za kisheria katika mwenendo wa kesi hiyo.
Badala yake Mahakama hiyo imeamuru kesi hiyo isikilizwe upya Mahakama Kuu kwa mujibu wa sheria, mbele ya Jaji mwingine.
Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo kutokana na rufaa waliyoikata warufani Masanja Magishi, Kamuga Ntemi, Lulenganija Lwinza na Semi Nhugijo.
Hata hivyo imeamuru warufani hao kusalia kizuizini wakisubiri kesi yao kusikilizwa upya.
Awali Masanja na wenzake, walihukumiwa adhabu hiyo baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la mauaji ya Shinje Gadi.
Katika kesi ya jinai namba 36 ya mwaka 2020 walidaiwa kutenda kosa hilo Oktoba 13,2018 katika Kijiji cha Igonda, wilaya ya Sumbawanga, kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu.
Walikata rufaa iliyosikilizwa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani walioketi Sumbawanga, Barke Sehel (kiongozi wa jopo), Dk Paul Kihwelo na Gerson Mdemu.
Katika hukumu ya rufaa hiyo ya jinai namba 286 ya mwaka 2021 majaji hao wamesema kuwa wamebaini mapungufu ya kisheria yaliyojitokeza wakati kesi inasikilizwa Mahakama Kuu.
Katika hukumu hiyo iliyoandikwa na Jaji Sehel, kwa niaba ya jopo hilo, Mahakama hiyo imesema kuwa baada ya kusikiliza hoja kutoka kwa mawakili wa pande zote na kupitia kumbukumbu za rufaa, wanakubali kwamba warufani hawakupewa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika kesi dhidi yao.
Jaji Sehel alitolea mfano wakati shahidi wa tatu alipokuwa akitaka kuwasilisha maelezo ya onyo ya Masanja, Wakili Mathias Budodi aliyekuwa akiwawakilisha warufani wote wanne aliyapinga, Mahakama ikasimamisha kesi ya msingi na kusikiliza kesi ndogo ya pingamizi hilo.
Amesema wakati kesi ndogo inasikilizwa mrufani wa pili hadi wa nne hawakupewa nafasi kuuliza swali lolote kwa mashahidi wa upande wa mashitaka na wa utetezi, ingawa maelezo hayo yalikuwa na madhara kwa masilahi yao.
Amesema kuwa hiyo ilifanyika kwa sababu wakili alikuwa anawawakilisha wote wanne.
Jaji ameongeza kuwa mbali na pingamizi la Masanja, pia mrufani wa tatu (Lugenganija) naye aliweka pingamizi la kupokelewa kwa maelezo yake ya onyo ambayo yalihusisha mrufani wa pili na nne (Kamuga na Semi).
“Kwa kuwa warufani wote walikuwa wakiwakilishwa na wakili mmoja, mshtakiwa wa pili na nne hawakuweza kuuliza maswali yoyote kwa mashahidi wa upande wa mashitaka na wa utetezi, ingawa maelezo yaliyokuwa karibu kupokelewa yalikuwa na madhara kwa masilahi yao,”amesema.
Jaji Sehel amesema kutokana na upungufu huo wa kushindwa kuwapa haki mrufani wa pili na nne ya kuwahoji mashahidi wa pande zote mbili pamoja na makosa mengine, Mahakama inaona kesi ya warufani haikuwa ya haki.
“Kwa kuzingatia sheria iliyosuluhishwa, tuna maoni thabiti kwamba uamuzi wa mahakama ya awali ulifikiwa kwa kukiuka haki ya kikatiba ya mrufani kusikilizwa na haiwezi kuruhusiwa kusimama,” amesema.
Hivyo kutokana na kasoro hiyo Mahakama hiyo imebatilishwa mwenendo wa kesi hiyo na imeitengua hukumu iliyotolewa, kwa masilahi ya haki na kwamba inaamuru warufani wasikilizwe upya mbele ya jaji mwingine.
Pia imeamuru kuwa wakati warufani wataendelea kubaki rumande wakisubiri kusikilizwa upya, pia itakapokuwa inasikilizwa kila mrufani awe na wakili wake ili waweze kuwa na uwakilishi wa kisheria.
Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo warufani hao waliwakilishwa na mawakili wanne wakiongozwa na Deogratius Sanga ambapo waliwasilisha sababu tatu za rufaa, huku upande wa jamhuri ukiwakilishwa na mawakili wawili wa Serikali waandamizi wakiongozwa na Safi Kashindi.
Katika sababu hizo za rufaa kwanza walidai kuwa kesi ya upande wa mashitaka haikuthibitishwa bila kuacha shaka kama inavyotakiwa kisheria, ambapo jaji alikosea kuwatia hatiani kutokana na ushahidi ambao unakinzana na hati ya mashitaka.
Sababu ya tatu walidai kuwa jaji alitumia kimakosa kanuni ya ushahidi wa kimazingira kuwatia hatiani.
Wakifafanua sababu hizo za rufaa, mawakili hao wa warufani waliieleza mahakama kuwa wateja hao hawakupewa haki ya kusikilizwa kwa kuwahoji mashahidi wa kila mmoja wao.
Walidai kuwa kesi ya mashitaka kwa kuzingatia maelezo ya onyo waliyotoa warufani hao mbele ya Polisi na ya ungamo mbele ya Mlinzi wa Amani (hakimu wa Mahakama ya Mwanzo), kila mmoja anadaiwa kumtaja mwenzake.
Hata hivyo wakati wa usikilizwaji hawakupewa nafasi ya kuuliza maswali kwa washitakiwa wenzao waliotoa ushahidi dhidi yao.
Hivyo mawakili hao walieleza kuwa ukiukwaji huo unasababisha shauri hilo kuwa batili na wakaomba mahakama ibatilishe mwenendo, hukumu na iamuru kesi hiyo ianze upya kwa mujibu wa sheria.