Hizi hapa tabia zitakazokuwezesha kuwa na furaha maishani

Kila mmoja wetu maishani huhangaika kwa namna yoyote ile kuhakikisha anakuwa na furaha. Wengine wala hawajali kama atatumia njia nzuri au mbaya, njia inayopendwa au isiyopendwa, njia inayoumiza au isiyoumiza wengine, atafanya chochote tu ilimradi awe na furaha.

Wapo ambao mtazamo wao ni kwamba ili uwe na furaha lazima uhakikishe una pesa nyingi. Watu wa namna hii mali na ukwasi ndio chanzo kikuu cha furaha. Bahati mbaya wengi walipambana kutafuta mali na pesa na walipovipata wakajikuta bado hawana furaha na mbaya zaidi yako mambo waliyoyafanya kwenye safari yao ya kuzitafuta pesa yamewaongezea maumivu ya moyo na majuto.

Ukichunguza maisha ya watu wengi wenye mitazamo kama hii utakuja kugundua kwamba mali, pesa na ukwasi sio chanzo cha furaha kabisa, badala yake vinaweza kukuondolea hata ile furaha kidogo uliyowahi kuwa nayo. Vipo vitu au zipo tabia ukiwa nazo ndizo zinakuwa chanzo cha kukuwekea mazingira ya fura maishani kwako na ukiwa na hizo hata unapopata pesa unaifurahia pesa yako, maana misingi ya furaha tayari ipo.

Katika makala hii nimeandika baadhi ya tabia ambazo kwa kuziishi utajiwekea mazingira makubwa ya kuwa na furaha.

Jenga tabia ya kuwa jasiri. Uliza, ongea, jieleze, ukikosea jirekebishe halafu songa mbele. Hofu yako ndio kitanzi chako maishani. Ukiona kuna kitu unakihofia hembu jiulize, nakihofia kwa nini na ili nini? Tabia ya kuhofu itakuwa kama ukuta wa kukuzuia kwenye kila hatua unayotaka kuichukua kwenye maisha yako. Jitie moyo, jiambie ninaweza na endelea kujaribu vile vitu ambavyo ulikuwa unavihofia. Taratibu utajikuta unaweza kuvifanya na muda kidogo utasherehekea sherehe za kuupata ujasiri. Hapo unakuwa umeushika ufunguo wa furaha yako.

Kwa nini unachukiana na watu? Kwa nini una maadui wengi? Shida ni wao au shida ni wewe? Ukiona una hasira na watu wengi, una chuki na migogoro na watu wengi, basi fahamu kwamba kuna uwezekano mkubwa kwamba shida ipo kwako na siyo wao. Yaani unawachukia hata wasiokuchukia? Ili nini sasa? Utapata faida gani?

Jinsi unavyojibebesha mizigo ya chuki na vinyongo ndivyo unavyojiongezea uzito wa kuruka kuelekea mafanikio yako. Jifunze kusamehe, kusahau na kuwaachilia wote uliowabeba moyoni mwako kwa sababu kamwe huwezi kuwa mtu mwenye furaha wakati moyoni mwako umewabeba watu kwenye machungu.

Jenga tabia ya kuwa mtoaji

Jenga tabia ya kuwa mtoaji, mtu mwenye kupendelea kuwapa watu au kuwasaidia watu wengine mahitaji yao. Toa bila kuangalia kama wewe utapewa, au utarejeshewa, toa bila kutegemea. Huna haja ya kuwasaidia walio karibu yako pekee, vipi kuhusu wale usiowajua kabisa? Vipi kuhusu wale wasiotegemea kabisa kama ungewasaidia? Ni baraka kubwa unapogusa maisha ya mtu ambaye wala hakuwahi kudhania ungemwona na kumsaidia.

Hii ndiyo maana halisi ya hadithi ya msamaria mwema inayozungumzwa kwenye maandiko matakatifu. Tafiti zinasema kwamba watu wenye tabia ya kusaidia watu “philanthropists” ni watu wenye furaha na utoshelevu mkubwa maishani. Hata wewe unaweza kuwa mmoja wao. Sio lazima uwe na kila kitu, la hasha. Kila mmoja ana cha kumsaidia mwingine.

Usiwe na mategemeo makubwa

Najua kabisa kwamba maisha hutufundisha kutegemea au kutazamia kutoka kwa wale wanaotuzunguka. Unatazamia jambo au mambo fulani kutoka kwa wazazi wako, Rafiki yako, mpenzi wako, jirani yako, mfanyakazi mwenzako, bosi wako na wengine wengi. Hii ipo kama kawaida. Shida kubwa inakuja pale ambapo unategemea na kutazamia kupitiliza, pale unapokuwa na matarajio makubwa kuliko uwezo wa huyo au hao unaowategemea kufanya unachokitegemea.

Ni sawa na kukaa kitako ujiandae kumkamua ng’ombe ambaye unatarajia atatoa lita 20 za maziwa halafu kumbe uwezo wa ng’ombe huyo ni kutoa lita 3 tu. Utaishia kukasirika, kuumia na kuwa na msongo wa mawazo. Kuwa na matarajio makubwa kupitiliza ni chanzo kimojawapo cha msongo wa mawazo kwenye maisha. Wewe tenda mema na fanya yaliyo mema bila kutarajia chochote.

Jifunze na jitahidi kuishi maisha rahisi. Kuwa mnyenyekevu kwa kila mtu, usijitweze wala kuwanyanyulia watu mabega kwa sababu eti ya nafasi yako, cheo chako, elimu yako, ujuzi wako, umaarufu wako au pesa zako. Kuwa mtu unayeweza kuishi maisha yoyote na wakati wowote. Usijione kuwa wewe ni wa juu sana na ukajitenga na wengi. Unawahitaji watu na wao wanakuhitaji wewe. Unanihitaji na mimi nakuhitaji. Unaweza usinihitaji leo, lakini ukanihitaji kesho. Usiige maisha ya mtu, ishi maisha yako mwenyewe. Sisemi usijifunze kutoka kwa watu, la hasha, kujifunza ni vema sana ila usiige kila kitu. Ishi kiuhalisia na acha kuishi maisha ya mitandaoni na maisha ya kwenye halaiki. Kuwa halisia, itakupunguzia msongo wa mawazo na gharama zisizo za lazima.

Ukijitahidi kuishi kwenye tabia hizi, mafanikio na furaha itakuwa sehemu kubwa ya maisha yako. Nakutakia maisha yenye furaha.

Related Posts