KICHAPO cha mabao 2-1, ilichokipata African Sports wiki iliyopita dhidi ya Stand United, kimemfanya kocha mkuu wa kikosi hicho, Kessy Abdallah kudai sababu zilizowanyima ushindi ni kutokana na wachezaji kukosa utulivu wa kumalizia nafasi.
Kessy amezungumza hayo baada ya timu hiyo kupoteza michezo saba kati ya tisa iliyocheza baada ya kushinda mmoja na sare moja pia, jambo linalomfanya kocha huyo kukiri wako katika wakati mgumu, ingawa anaamini bado wana nafasi huko mbeleni.
“Licha ya kutawala mchezo ila tumepoteza kwa sababu ya kukosa umakini wa kumalizia nafasi tulizozipata, bado tuna kazi kubwa ya kufanya, ili kuhakikisha tunarekebisha changamoto hiyo kwa haraka zaidi na kuendana na ushindani,” alisema.
Kocha huyo aliongeza, bado hakuna balansi nzuri ya kuzuia na kushambulia hivyo anarudi katika uwanja wa mazoezi kufanyia kazi changamoto hiyo, huku akiwaomba mashabiki kukipatia sapoti kikosi hicho akiamini bado ni mapema kuwakatia tamaa.
Timu hiyo ambayo ni mabingwa wa Kombe la Muungano mwaka 1988, imepanda Ligi ya Championship msimu huu baada ya kushuka daraja msimu wa 2022-2023 iliposhika nafasi ya 14 na pointi 23, huku msimu uliopita ikiwa ndio mabingwa wa First League.