WAKATI Golikipa wa Yanga na timu ya taifa ya Mali, Djigui Diarra akiwa tegemezi kwenye kikosi cha wananchi, Kinda la Tanzania, James Octavian anakiwasha kwenye akademi ya ABM Foot.
Nyota huyo anacheza nafasi mbalimbali uwanjani kiungo mshambuliaji, winga na kiungo mkabaji akiwa na uwezo wa kucheza namba zote kwa ufasaha.
Akizungumza na Mwanaspoti, Octavian alisema wapo watanzania saba kwenye akademi hiyo ya vijana chini ya miaka 18 na kila mmoja anapata nafasi ya kucheza.
Ilivyokuwa hadi anafika Mali, walikuja mawakala Tanzania kutafuta vipaji na Octavian akiwa miongoni mwa vijana saba waliofanikisha kupita kwenye mchujo huo.
Aliongeza kuwa alichukuliwa akiwa kwenye akademi ya Morogoro Soccer iliyopo mkoani humo na anatimiza mwaka sasa tangu ajiunge nao.
“Huku hatupati shida kwa sababu kila kitu tunahudumiwa na akademi kama timu tu, na sio Tanzania tu bali wapo wachezaji wengine kutoka mataifa mbalimbali,” alisema na kuongeza
“Kama mchezaji unakuwa na malengo kwa hapa nilipofika nikiongeza juhudi tu naamini nitafanikiwa kama ilivyo kwa Mbwana Samatta kucheza ligi kubwa Ulaya.”