KIUNGO mkabaji nyota anayekipiga Tottenham Hotspur iliyopo Ligi Kuu England (EPL), Yves Bissouma amesema kipa wa Yanga, Djigui Diarra ni kipa bora kwa sasa duniani.
Diarra na timu yake ya Mali imefuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika Morocco.
Ikumbukwe Diarra mbali na kuwa kipa tegemeo katika kikosi cha Yanga, lakini hata kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Mali.
Kupitia ukurasa wa Instagram wa Bissouma aliandika maandishi kwa lugha ya kifaransa yenye maana ya kumpongeza Diarra akiambatanisha na picha ya nyota huyo.
Maneno hayo yalisomeka hivi; “Mlinzi bora duniani, sitaki kujua chochote,” akiandika muda mchache baada ya timu hiyo kufuzu AFCON.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 28 kabla ya kutua Spurs mwaka 2022 akitokea Brighton & Hove Albion inayoshiriki pia EPL, amewahi kukipiga Real Bamako ya Mali, Lille II na Lille zote za Ufaransa.