KOCHA Mkuu wa Bravos do Maquis ya Angola, Mario Soares, amesema wanapaswa kujiandaa vyema na mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi dhidi ya Simba, utakaopigwa Novemba 28 mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Soares amezungumza hayo kutokana na mwenendo usioridhisha wa kikosi chake katika Ligi Kuu ya Angola maarufu Girabola, huku akiwataka wachezaji wa timu hiyo kujiandaa kimwili na kisaikolojia wakati watakapopambana na Simba.
“Tuko katika kundi gumu kutokana na aina ya wapinzani tuliokuwa nao, ni kweli tumekuwa na mwenendo usioridhisha ila haya ni mashindano tofauti na hata namna ya uchezaji na maandalizi kwa ujumla yanabadilika, tunawaheshimu kila mmoja wetu,” alisema kocha huyo.
Akizungumzia ubora wa Simba msimu huu, Soares alisema timu hiyo ina wachezaji bora ambao wamekuwa wakicheza kitimu zaidi bila kujali mmoja mmoja, hivyo anaiheshimu kutokana na kiwango ilichojiwekea, hasa inaposhiriki michuano ya kimataifa.
“Siwezi kusema mchezaji mmoja mmoja kwa sababu ukiangalia wanacheza kwa umoja ndio maana wanaongoza Ligi Kuu, huu utakuwa mchezo mzuri na mgumu kwa kila upande, ingawa tunapaswa kuongeza umakini kuanzia uzuiaji na ushambuliaji pia,” alisema Soares.
Timu hizo zimepangwa Kundi A katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika zikiwa na CS Constantine ya Algeria na CS Sfaxien ya Tunisia.
Simba iliyopo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi 25 baada ya kucheza 10, imeshinda minane, sare mmoja na kupoteza mmoja, ikifunga mabao 21 na kuruhusu 3, ikiwa na wastani mzuri tofauti na wapinzani wao katika kundi lake.
Katika kikosi cha Simba, Jean Charles Ahoua mpaka sasa amehusika kwenye mabao mengi (9) kati ya 21 yaliyofungwa na timu hiyo kwenye ligi kutokana na kufunga manne na asisti tano.
Kwa upande wa Bravos katika Ligi Kuu ya Angola ‘Girabola’ imecheza michezo kumi kabla ya ule wa jana dhidi ya CD Lunda Sul ambapo kati ya hiyo imeshinda mitatu tu, sare tano na kupoteza miwili, ikishika nafasi ya sita na pointi zake 14.
Katika michezo hiyo, kikosi hicho kimefunga mabao 11 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 10, jambo linaloonyesha wazi hakipo vizuri maeneo mawili ya ushambuliaji na uzuiaji, kitu kinachoweza kuipa faida Simba itakapokutana nayo.
Bravo inarejea tena Dar es Salaam msimu huu baada ya mchezo wa awali wa marudiano wa michuano hiyo kutoka suluhu na Coastal Union uliochezwa Agosti 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, hivyo kufuzu hatua inayofuatia kwa jumla ya mabao 3-0 kutokana na ushindi huo wa nyumbani. Pia ikaenda kuiondosha Saint Eloi Lupopo kwa jumla ya mabao 3-1 na kufuzu makundi.