Jengo hilo lenye ghorofa nne lilianguka takriban saa 3:00 asubuhi (saa 12:00 GMT) Jumamosi katika soko lenye shughuli nyingi la Kariakoo katikati ya mji mkuu wa kibiashara, Dar es Salaam.
Watu 13 wamethibitishwa kufariki kutokana na kuporomoka kwa janga hilo, kikosi cha zima moto kilisema. Watu wasiopungua 84 walikuwa wameokolewa wakiwa hai kutoka kwenye eneo la tukio.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alisema Jumapili kuwa bado kuna watu zaidi waliokwama kwenye sakafu ya chini ya jengo lililoporomoka, bila kutaja idadi yao.
“Tunawasiliana… na tayari tumewapa oksijeni na maji,” alisema. “Wako salama na tunaamini wataokolewa wakiwa hai na salama.”
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amezungumza Jumapili na vyombo vya Habari akiwa Brazil alikokwenda ziarani kikazi.
“Hadi sasa hatujajua sababu za kuanguka kwa jengo Hilo kwa sababh kipaumbele chetu kilikuwa ni kuwaokoa walionaswa katika jengo hilo” amesema Rais,
Juhudi za uokozi zakwaa kisiki
Mkuu wa kikosi cha zima moto, John Masunga, alisema juhudi za kutafuta na kuokoa zimekwamishwa na kuta nyingi zilizokuwa sehemu ya jengo hilo.
Baada ya sakafu za jengo hilo kuporomoka kwa kasi hadi zikaunda mlima wa vifusi, mamia ya watoa huduma ya kwanza walitumia nyundo na mikono yao kuvunja mawe kwa saa kadhaa. Baadaye, kreni na vifaa vingine vizito vya kuinua vililetwa kusaidia.
Haijabainika wazi ni kwa nini jengo hilo la biashara liliporomoka, lakini mashuhuda waliviambia vyombo vya habari vya ndani kuwa ujenzi wa kuongeza nafasi ya biashara chini ya ardhi ulianza Ijumaa.
Tukio hilo limeibua tena ukosoaji juu ya ujenzi usiodhibitiwa katika jiji hilo la Bahari ya Hindi lenye wakazi zaidi ya milioni tano.
Moja ya miji inayokua kwa kasi zaidi duniani, Dar es Salaam imeshuhudia ongezeko la biashara ya nyumba, huku majengo yakijengwa kwa kasi bila kujali sana kanuni za ujenzi.
Mwaka 2013, jengo lenye ghorofa 16 lilianguka jijini Dar es Salaam, na kusababisha vifo vya watu 34.
Florence Majani amechangia Ripoti hii kutoka Dar es Salaam