Miili zaidi yapatikana ajali ya jengo Dar es Salaam – DW – 17.11.2024

Kwa siku ya pili mfululizo, waokoaji katika taifa hilo la Afrika Mashariki wamekuwa wakichimba kwenye kifusi cha jengo lililoporomoka siku ya Jumamosi (Novemba 16), wakitarajia kuwapata manusura zaidi waliokwama chini.

Jengo hilo la ghorofa nne lilianguka majira ya saa 3:00 asubuhi katika mtaa wenye shughuli nyingi wa Kariakoo, kitovu kabisa pa shughuli za kibiashara kwenye jiji hilo la bandari. 

Kufikia mchana wa Jumapili, idadi ya waliothibitishwa kupoteza maisha walikuwa watano, huku wengine 70 wakiwa wameokolewa wakiwa hai, kwa mujibu wa kikosi cha zimamoto.

Soma zaidi: Jengo laporomoka na kuuwa kadhaa Kariakoo Dar es Salaam

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alisema bado kuna watu wengi kwenye ghorofa ya chini ya jengo hilo bila kutaja idadi kamili.

“Tunawasiliana nao na tayari tumewapatia oksijini na maji,” alisema, akiongeza kwamba: “Wako salama na tunaamini tuwaokowa wakiwa hai na wazima.”

Mkuu wa kikosi cha zimamoto, John Masunga, alisema msako na uokoaji unakabiliwa na kuna kuwapo na kuta nyingi kwenye jengo hilo.

Kutokana na ghorofa za jengo hilo kuporomoka na kulaliana na kuunda mlima wa vifusi, mamia ya wananchi na waokoaji walilazimika kutumia vifaa hafifu na hata mikono mitupu kuondoa vifusi kwa masaa kadhaa kabla ya kufikia walipokwama watu.

Ujenzi holela, uokoaji mgumu

Makreni na vifaa vyengine vizito vya uokoaji vililetwa baadayae kwa ajili ya kusaidia uokoaji.

Dar es Salaam Tanzania
Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, akizungumza kwenye eneo la tukio.Picha: Eric Boniphace/DW

Bado haijafahamika sababu ya kuporomoka kwa jengo hilo lililokuwa na maduka mengi lakini mashahidi waliviambia vyombo vya habari kwamba kulikuwa na ujenzi wa wa kuitanuwa ghorofa ya chini kwa ajili ya maduka zaidi ulioanza siku ya Ijumaa (Novemba 15).

Soma zaidi: Jengo laporomoka Kariakoo, Dar es Salaam

Tukio hili limeibua upya ukosoaji dhidi ya ujenzi usiofuata taratibu kwenye mji wa Bahari ya Hindi wenye wakaazi zaidi ya milioni tano.

Ukiwa mmojawapo wa miji inayokuwa kwa kasi, Dar es Salaam imekuwa sehemu inayoshuhudia kupanda kwa ujenzi wa majengo ya anasa na ya kibiashara, lakini mara nyingi unaoikuka kanuni za majengo salama.

Mnamo mwaka 2016, jengo la ghorofa 16 liliporomoka kwenye mji huo na kuuwa watu 34.

Related Posts