STRAIKA wa zamani wa Fleetwoods United FC inayoshiriki Ligi ya Daraja la Pili UAE, Mtanzania Mgaya Ally amerudi Tanzania kucheza Ligi Kuu ili kupata dili la Uhispania.
Nyota huyo alimaliza mkataba wa miaka miwili hivi karibuni na kabla ya kucheza Falme za Kiarabuni aliwahi kutumikia Coastal Union ya vijana U-20 msimu wa 2020/21.
Akizungumza na Nje ya Bongo, Mgaya alisema analazimika kurudi kutafuta timu bongo dirisha hili dogo kutokana na ofa aliyopata Uhispania inayohitaji ili acheze huku awe angalau amecheza Ligi Kuu na kuitwa timu ya taifa.
Mgaya alisema hadi sasa bado hajapata timu bongo akiamini kucheza Ligi Kuu kutamfanya abadilishe maisha kutokana na ofa nono aliyowekea mezani.
“Hispania ili nicheze nahitajika angalau nimetumika kweye klabu za nyumbani kwa simu angalau mmoja na timu ya taifa, ndio napambana kuhakikisha hilo linafanikiwa kwa sasa nipo kwetu napumzika kidogo hadi dirisha dogo,” alisema Mgaya.
Kabla ya kupata Hispania mshambuliaji huyo alikuwa na ofa tatu kutoka Oman, Kazakhstan na Jordan zimeondoka? hapa anajibu.
“Ni kweli bado zipo naendelea kufanya mawasiliano nao na kama Hispania ikishindikana basi nitarudi kuangalia hizo nchi tatu mojawapo nitakayojiunga nayo.”