Mwendokasi chanzo ajali iliyoua, kujeruhi 10 Geita

Geita. Mwendokasi na dereva wa gari binafsi aina ya Kluger kutozingatia sheria za usalama barabarani imetajwa kuwa chanzo cha ajali iliyotokea eneo la Mpomvu Kata ya Mtakuja mjini Geita, na kusababisha kifo cha mtu mmoja na majeruhi 10.

Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita imeeleza ajali hiyo iliyotokea jana Jumamosi, Novemba 17, 2024 ilisababishwa na dereva wa gari  dogo iliyokuwa ikitokea Katoro kwenda Geita kuendesha kwa mwendo kasi na kugongana uso kwa uso na gari ya abiria aina ya Tata iliyokuwa ikitokea Geita kuelekea Katoro.

Shuhuda wa ajali hiyo, Jacob Paul amesema dereva wa gari dogo alikuwa kwenye mwendokasi na alipofika eneo hilo, gari lilimshinda na kuhama barabara na kwenda kugongana uso kwa uso na basi hilo la abiria.

“Tulipokuwa tunawatoa mmoja alifia eneo la ajali wengine walioumia sana ni wale waliokuwa kwenye Kluger, tuliwasaidia japo miguu ilikuwa imevunjika na eneo la tumbo dereva alikuwa ameumia sana ndio askari wakaja wakawachukua na kuwapeleka hospitali,” amesema.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita, Brian Kimario amesema walipokea majeruhi wawili waliohamishwa kutoka Hospitali ya Mji Geita ambao walikuwa kwenye hali mbaya kutokana na majeraha waliyoyapata.

“Tulipokea majeruhi wawili ambao ni  Dismas Mlashani aliyekua amevunjika miguu na kuvujia damu kwenye tumbo na Shija Ihano ambaye naye alikua amevunjika miguu, tuliwafanyia huduma usiku ule ule na kwa sasa wanaendelea vizuri mmoja bado yupo ICU,“ amesema Dk Kimario.

Mmoja wa majeruhi, Shija Ihano ambaye ni mfanyabiashara wa madini ya dhahabu akizungumza akiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa amesema alitokea kwenye mgodi wa Biharamulo kwenye shughuli zao za uchimbaji.

“Tulipofika Katoro tulitulia tukala na kuanza tena safari, alikua anaendesha mwenzangu nikapata usingizi nikajilaza nimekuja kushituka watu wananisaidia miguu yote imevunjika ndio madaktari wakaja kutuchukua,” amesema.

Amesema walikuwa wakielekea Msalala wilayani Nyang’hwale kwa shughuli zao za madini na kwenye gari alikuwa na zaidi ya Sh8.3 milioni pamoja na kiasi cha madini ya dhahabu waliyokuwa wametoka nayo kwenye mgodi wa Biharamulo na hafahamu zilipo ikiwamo simu zake tatu.

Related Posts