Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema hadi saa 4:00 asubuhi ya leo Jumapili, Novemba 17, 2024 watu 13 walikuwa wamepoteza maisha na majeruhi 84 kuokolewa katika ghorofa lililoporomoka, Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Pia ametoa maagizo kwa Waziri Mkuu na Polisi, “Namtaka Waziri Mkuu kuongoza timu ya ukaguzi majengo kuendelea na zoezi la kukagua majengo yote ya Kariakoo tupate taarifa kamili ya hali ya majengo ya Kariakoo ilivyo. Jeshi la Polisi ipate taarifa kamili kwa mmiliki wa jengo ya jinsi ujenzi ulivyokuwa,” amesema.
Rais Samia amesema hayo leo Jumapili, akiwa Rio de Janeiro, Brazil kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu ya Tanzania. Amesema kati ya majeruhi hao 26 wanaendelea na matibabu.
“Serikali itabeba gharama za matibabu kwa waliojeruhiwa na kuhakikisha waliopoteza maisha wanastiriwa ipasavyo, nitoe pole kwa ndugu, jamaa na marafiki,” amesema Rais Samia.
Amesema Serikali itaendelea kutoa taarifa zaidi, ”hadi sasa sababu za kitaalamu za jengo kuporomoka hazijachunguzwa na kubainishwa na kipaumbele chetu ni kufanya uokozi.”
Rais Samia amesema taarifa zote hizo zikipatikana zitawekwa wazi na Watanzania watazisikia.
Endelea kufuatilia Mwananchi.