Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema mpaka Jana jumla ya watu waliofariki dunia kutokana na kuporomo ka kwa jengo la ghorofa Kariakoo ilikuwa ni wanne huku sababu ikiwa sio kukosa hewa.
Chalamila ameyasema hayo leo Jumapili Novemba 17, 2024 wakati shughuli za uokozi zikiendelea katika jengo hilo lililoporomoka jana Jumamosi Novemba16, 2024.
“Mpaka mudu huu waliokufa kwa safocation (kukosa hewa) hatuna taarifa hiyo na hii ni kwa taarifa ya papo kwa hapo,”amesema Chalamila.
Pia, amesema wanaendelea kuwasiliana na watu waliokwama chini ya jengo hilo na wamepelekewa gesi, maji na glucose huku wakiwaomba kuendelea kuwa wastahimilivu.
Aidha, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), imetoa orodha ya majina 40 ya manusura wa ajali ya jengo la ghorofa kuporomoka Kariakoo waliopelekwa hospitalini hapo kwa matibabu.
Katika taarifa hiyo iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa hospitali hiyo, Aminiel Aligaesha, imesema hadi ilipotimu saa 11 jioni jana, manusura 35 waliruhusiwa kurudi nyumbani.
Mrakibu Mwandamizi Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Peter Mtui, amesema hadi sasa (jana jionia) watu watano wamepoteza maisha huku wengine 42 wakijeruhiwa.
Shughuli ya kufukua kifusi inaendelea katika jengo hilo la ghorofa nne lililoporomoka asubuhi ya Jumamosi Novemba 16, 2024 katika eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Endelea kufuatilia Mwananchi.