RC Mwanza azindua Ilemela Nyamachoma Festival – Burudani ya Kipekee kwa Wafanyabiashara na Wananchi wa Mwanza

NA BALTAZAR MASHAKA, ILEMELA

Serikali ya Mkoa wa Mwanza imezindua Tamasha la Nyamachoma, maarufu kama Ilemela Nyamachoma Festival, litakalofanyika kila Jumamosi katika viwanja vya Nane Nane, Kata ya Nyamhongolo, Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.

Tamasha hilo linatarajiwa kuwa na manufaa makubwa kiuchumi kwa Mkoa wa Mwanza, huku likilenga kukuza biashara, kutoa nafasi kwa wafanyabiashara kuonesha bidhaa zao, na kuongeza mapato ya halmashauri.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa tamasha hilo leo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amesema kuwa tamasha hili litainua kipato cha wafanyabiashara wa eneo hilo na kusaidia kuongeza vyanzo vya mapato vya Halmashauri, jambo litakalosaidia kuboresha huduma za jamii.

“Eneo hili linaendelea kutunzwa na kuboreshwa kwa ajili ya shughuli mbalimbali kama hizi. Shughuli hii iambatane na uwepo wa vyakula vya asili na nyama pori zenye vibali maalum, najua watu wengi wanapenda kuonja radha ya nyama pori,” amesema Mtanda.

Pia ametoa wito kwa Halmashauri ya Ilemela kuandaa mashindano ya kuhamasisha ubunifu katika tamasha hili, ili kila mtu ajitahidi kutoa huduma bora zaidi na kuvutia wateja; “Tunataka tamasha hili liwe na ubunifu zaidi kila mwaka.”
Katika hatua nyingine, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Elikana Balandya, amesisitiza kuwa tamasha hili ni tukio muhimu kwa maendeleo ya Mkoa wa Mwanza na Ilemela kwa ujumla.

Ameunga mkono wazo la kuwa na vyakula vya asili, akisema kuwa hiyo itavutia watalii wa ndani na nje ya nchi; “Kuna nyama aina ya Ng’omele imepotea, hivyo tukiwa na vyakula vya asili na ngoma za asili, tamasha litapendeza zaidi na kuvutia hata watalii.”

Mbunge wa Ilemela, Dkt. Angeline Mabula, ametoa pongezi kwa kuanzishwa kwa tamasha hili na kumpongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, Ummy Wayayu, kwa ubunifu na jitihada za kuwakutanisha wafanyabiashara katika eneo hili.

“Ni jambo jema kuona viongozi wetu wanajitahidi kuleta maendeleo kwa kushirikiana na wananchi,” amesema Dkt. Mabula.

Katibu wa Wadau wa Ilemela Nyamachoma Festival, Ezra Shandu, ameeleza changamoto ya miundombinu ya eneo hilo, akitoa wito kwa halmashauri kuboresha miundombinu hasa wakati wa mvua ili kuepuka usumbufu kwa wateja na biashara, hivyo ni muhimu kushirikiana kati ya halmashauri na wadau mbalimbali ili kuboresha huduma za tamasha.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, Ummy Wayayu, amehakikishia wafanyabiashara kuwa tamasha hili ni endelevu na litakuwa na maboresho kila mwaka.

Amesema kuwa, pamoja na kuongeza mapato ya halmashauri, tamasha hili litakuwa sehemu ya kupumzikia na burudani kwa wananchi, na kusaidia kuboresha afya zao kwa kupunguza msongo wa mawazo.

Wakazi wa Ilemela pia walionyesha furaha yao kuhusu uzinduzi wa tamasha hili. Esther Masalu, mkazi wa Igoma, ameelezea furaha yake akisema; “Ni jambo jema kupata sehemu ya kupumzika, kula na kunywa huku tukibadilishana mawazo. Rai yangu ni kuwaongezea siku, ni furaha yangu kupata sehemu ya mtoko kila Jumamosi.

“Hivyo, kwa jumla Ilemela Nyamachoma Festival inaonekana kuwa ni tukio la kipekee linalolenga kuleta burudani, kukuza uchumi wa eneo hilo, na kutoa nafasi kwa wananchi na wafanyabiashara kuungana na kubadilishana mawazo.

 

Related Posts