CHAMA cha Riadha Mkoa wa Pwani kimepata viongozi wapya watakaokiongoza kwa miaka minne, akiwamo Mwandishi wa Habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), Imani Makongoro.
Uchaguzi huo umefanyika juzi na kusimamiwa na Ofisa Michezo wa Kibaha mjini, Burwan Tilusubya, ukihusisha wajumbe 14 waliopiga kura kutoka wilaya za Bagamoyo, Chalinze, Kibiti, Kisarawe, Mkuranga, Rufiji na Kibaha.
Viongozi waliochaguliwa ni Robert Kalyahe aliyeshinda nafasi ya uenyekiti kwa kura za ndiyo 14, idadi sawa na aliyopata Imani Makongoro katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti.
Imani pia ni Katibu Msaidizi Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (Taswa).
Katika uchaguzi huo, nafasi ya Katibu Mkuu alishinda, Elias Daniel kwa kura 13 za ndiyo na moja ya hapana, huku Katibu Msaidizi alishinda Godfrey Haule kwa kura 14, huku Atson Mbugi akishinda katika nafasi ya Mweka hazina kwa kura 13 za ndiyo na moja ya hapana.
Lydia Masena alishinda nafasi ya Mwakilishi wa Wanawake katika Mkutano Mkuu, huku Jilala Mwandu akishinda nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu.
Nafasi za Wajumbe wa Kamati ya Utendaji zilienda kwa Seleman Idd, Rajabu Rashid, Ndimbumi Ifuge, Mwanamwema Komba, Happiness Mbago na Emarensiana Mtimbi.
Mwenyekiti wa uchaguzi huo, Burwan Tilusubya alitaka uongozi mpya uliochaguliwa kuendelea kuijenga riadha kwenye mkoa huo.
Mwenyekiti mpya, Robert Kalyahe alisema dhamana waliyopewa wataitendea haki na kuendeleza rekodi ya mkoa wa Pwani kwenye riadha. “Pwani inakwenda kuwa jicho la riadha Tanzania, tumekuwa na rekodi ya kufanya vizuri kwenye mashindano ya Taifa katika tatu bora miaka mingi. Mikakati tuliyonayo ni kuwa kinara wa riadha nchini,” amesema Kalyahe.